Michezo

Wanaomtaka Sancho wamnunue kabla ya Agosti 10 – Dortmund

August 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BORUSSIA Dortmund wameweka Agosti 10, 2020 kuwa siku ya mwisho kwa kikosi chochote kinachohemea huduma za chipukizi Jadon Sancho anayehusishwa pakubwa na Manchester United kumsajili rasmi.

Dortmund inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) wamewaambia Man-United kwamba watalazimika kuweka mezani zaidi ya Sh14 bilioni ili kujinasia huduma za Sancho, 20.

Bado hakuna maafikiano yoyote miongoni mwa vinara wa Dortmund kuhusu iwapo fedha za mauzo ya Sancho zitalipwa kwa mkupuo au kwa awamu.

Dortmund wameweka makataa hayo kwa kuwa wasimamizi wamekariri kwamba hawatataka maandalizi yao kwa minajili ya msimu ujao wa 2020-21 katika Bundesliga kuvurugwa.

Msimu mpya wa Bundesliga umepangiwa kuanza Septemba 18 huku siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji ikiwa Oktoba 5, 2020.

Sancho amekuwa Dortmund kwa miaka mitatu baada ya kuagana na Manchester City kwa kima cha Sh1.4 bilioni mnamo Agosti 2017.

Mnamo Julai 2020, Dortmund waliwapiga kumbo Man-United katika vita vya kuwania maarifa ya kiungo chipukizi Jude Bellingham, 17, aliyeagana na Birmingham City kwa zaidi ya Sh4.2 bilioni.

Mwanzoni mwa msimu huu wa 2019-20, Dortmund pia walijinasia huduma za fowadi chipukizi kutoka Erling Braut Haaland aliyebanduka kambini mwa Red Bull Salzburg nchini Austria na kuyoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Dortmund licha ya kuhusishwa pakubwa na Man-United.