Habari MsetoSiasa

Wanaoniuliza maswali kuhusu 2022 wanikome – Raila

December 28th, 2018 2 min read

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ameonya wanaomsukuma atangaze iwapo atawania urais 2022 wakome, akisema akianza kampeni sasa miradi ya serikali itakwama.

“Nikianza kampeni sasa, mara moja nchi hii itakuwa katika hali ya kampeni kuanzia kesho na hakuna atakayekuwa akizungumza kuhusu ajenda nne kuu za maendeleo,” akasema Bw Odinga.

Maneno haya ya kiongozi huyo yaliashiria kuwa hata kama analenga kuwania urais tena, bado anataka kumpa nafasi Rais Uhuru Kenyatta kuwafanyia kazi Wakenya, hadi ‘wakati muafaka’ wa kuchapa siasa utakapofika.

Mapema wiki hii Bw Odinga alitoa matamshi ya kukanganya aliposema kuwa hatakuwa kwenye debe 2022 lakini baadaye akasema atatangaza msimamo wake wakati mwafaka ukifika.

Katika mahojiano cha televisheni cha Citizen, Bw Odinga alisisitiza umuhimu wa taifa kuachwa liungane, na serikali kufanya maendeleo kwanza, badala ya siasa za kila wakati.

Akijibu watu ambao wamekuwa wakidai kuwa muafaka baina yake na Rais Kenyatta unalenga kumjenga kwa ajili ya 2022, kiongozi huyo alisema kuwa watu hao bado hawaelewi vyema kilichowasukuma kuamua kuungana.

Alisema ameamua kuungana na Rais Kenyatta kupigia debe masuala ya umuhimu wa kitaifa kama kuunganisha Wakenya na kuleta amani na maendeleo.

Alisema hata kuungana kwao na Rais Kenyatta kulikuwa baada ya kuona namna taifa lilikuwa limetengana, huku hata vyombo vya habari vikichimba historia za utengano baina ya familia zao enzi za Mzee Jomo Kenyatta na Oginga Odinga ndipo wakaamua kuwa kielelezo kwa vizazi vijavyo.

Alisema japo kambi zote mbili, za Jubilee na NASA zilikuwa zimechukua misimamo mikali mwanzoni mwa mwaka huu, waliamua kuweka ubinafsi kando kwa manufaa ya taifa.

Hakuna anayefahamu kwa uhakika kilichowasukuma viongozi hao wawili kufanya uamuzi wa namna hiyo wakati walikuwa hawaonani macho kwa macho, wala walichoelewana faraghani kabla ya kujitokeza kwa umma.

Lakini muafaka wao siku za baadaye haukupokelewa vyema na baadhi ya wafuasi wakuu wa pande zote.

Lakini Bw Odinga na Rais wanasisitiza walipatana kwa ajili ya amani na umoja wa kitaifa.