Habari Mseto

'Wanaopigwa msasa kuongoza NLC ni wafisadi'

September 19th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge kuhusu Ardhi Alhamisi ilianza kuwapiga msasa watu tisa waliopendekezwa kwa nyadhifa za mwenyekiti na makamishna wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) huku maswali kuhusu ufaafu wao kimaadili yakiibuliwa.

Kamati hiyo ilipokea barua kutoka kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) ikisema kuwa Wakili Gershom Otachi aliyeteuliwa kwa wadhifa wa mwenyekiti wa tume hiyo hajakuwa akilipa ushuru ipasavyo.

Naye Profesa James K. Tuitoek aliyependekezwa kwa wadhifa wa kamishna alikabiliwa na madai kwamba alinyakua ekari tano ya ardhi ya Shirika la Ustawi wa Kilimo (ADC) katika eneo bunge la Magarini, kaunti ya Kilifi.

Aliyekuwa mbunge wa Nyeri Mjini Bi Esther Murugi alipohojiwa na bunge Septemba 19, 2019. Picha/ Charles Wasonga

Masuala hayo yalipelekea kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kitui Kusini Rachael Nyamai kuita Kamishna Mkuu wa KRA James Mburu na kaimu mkurugenzi wa ADC Mohammed Bulle kufika mbele yake Ijumaa kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo.

“Licha ya Bw Otachi kuwasilisha cheti ya uidhinisho wa ulipaji kodi, KRA jana (Jumatano), Septemba 18, 2019, aliwasilisha barua nyingine ikidai hajatimiza masharti ya ulipaji kodi. Hatujui nani msema kweli hapo,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt Rachael Nyamai.

Mtaalamu wa masuala ya ardhi, Bw Reginald Okumu alipofika mbele ya kamati hiyo. Picha/ Charles Wasonga

Lakini Bw Otachi ambaye ni mwenyekiti wa bodi Shirika la Ustawi wa Kawi ya Mvuke (GDC) alisisitiza kuwa cheti alichowasilisha kwa kamati hiyo ni halali kwani alipewa na KRA mnamo Juni 12/6/2019.

Naye Profesa Tuitoek aliwasilisha barua iliyotiwa saini na Bw Bulle akifafanua kuwa siye anayedai kunyakua ardhi ya ADC Magarini bali alikuwa ni Bw James C.Tuitoek.

Waziri wa zamani Kazungu Kambi. Picha/ Charles Wasonga

“Ama kwa kweli ADC imethibitisha kuwa mtuhumiwa wa unanyakuzi wa ardhi siyo mimi Profesa James K. Tuitoek bali ni James C. Tuitoek. Isitoshe, sielewi Magarini ni ni wapi,” akasema.

Wengine waliohojiwa Alhamisi ni aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Esther Murugi, Getrude Nguku, Bw Reginald Okumu na aliyekuwa mbunge wa Kaloleni na Waziri wa Leba Samuel Kazungu Kambi.