Habari Mseto

Wanaoshukiwa kuiba Sh75m waachiliwa kwa Sh1m kila mmoja

September 11th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA sita wa wizi wa Sh75.9 milioni za benki ya Standard (SCB) kimabavu Jumatano waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni kila mmoja na wadhamini wawili wa kiasi hicho.

Na wakati huo huo, hakimu mkuu Francis Andayi aliamuru Mamlaka Huru ya Polisi (IPOA) iwachunguze maafisa wa Polisi kutoka kitengo cha Flying Squad waliowatesa na kuwaumiza washukiwa hao sita.

Bw Andayi alisema inasikitisha sana kwa Polisi kuwatesa washukiwa ilhali sheria inakataza washukiwa kuteswa.

“Naamuru IPOA ichunguze madai kwamba maafisa wa polisi waliowatia nguvuni washukiwa waliwatesa washukiwa hao. Ripoti iwasilishwe kortini na Polisi wahusika wachukuliwe hatua kali,” Bw Andayi aliamuru.

Wakili Cliff Ombeta anayewatetea washtakiwa alielezea jinsi polisi waliwatesa na kuwaumiza.

Koplo Duncan Kavesa Luvuga alimwonyesha hakimu majeraha aliyopata alipopigwa , kuzamishwa majini, na kutiwa selotepu mdomoni na kufungwa kichwani kwa karatasi ya nailonu huku akilazimishwa kueleza alikoficha mgawo wake wa pesa hizo.

Bw Andayi alitoa agizo hilo alipowaachilia washtakiwa Konstebo Chris Machogu, Koplo Luvuga, Konstebo Boniface Mutua, Vincent Owuor, Alex Mutuku na Francis Muriuki.

Wakili Cliff Ombeta (kushoto) aonyesha hakimu majeraha ya Koplo Duncan Luvuga. Picha/ Richard Munguti

Aliamuru washukiwa wazuiliwe katika gereza la viwandani ambapo watakuwa wakitolewa kupelekwa kwa afisa wa uchunguzi wa jinai kituo cha polisi cha Langata kuwahoji kwa muda wa siku saba.

Washtakiwa hawa walikanusha mashtaka mawili ya wizi wa mabavu na kuharibu masanduku na vifaa vingine vya kampuni ya G4S zenye thamani ya Sh1,267,000.

Sita hao walikana mnamo Septemba 5, 2019 katika eneo la Nairobi West waliwanyang’anya wafanyakazi wa G4S waliwanyang’anya kimabavu Sh75,949,350.

Shtaka lilisema sita hao walikuwa wamejihami kwa silaha hatari walipotekeleza wizi huo.

Bw Andayi alitupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) la kuwanyima washukiwa hao dhamana akisema “ hajawasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kuwanyima washukiwa dhamana.”

Hakimu alimzomea afisa anayechunguza kesi hiyo kwa kuwasilisha mahakamani beti tisa za afidaviti ambazo hazielezei chochote kuhusu ombi la kuwanyima washukiwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka Bi Jacinta Nyamosi alisema washukiwa hao walitiwa nguvuni siku tofauti tofauti na mahala mbali mbali na wanahofiwa watawavuruga mashahidi.

Alisema pesa zilizoibwa hazijapatikana.