NA RICHARD MUNGUTI
WAHUDUMU 16 wa bodaboda waliofikishwa kortini kwa madai ya kumnyang’anya kimabavu afisa wa Ubalozi wa Zimbabwe simu iliyo na thamani ya Sh130,000 na kumdhalilisha kijinsia watazuiliwa kwa siku 15 ili polisi wakamilishe uchunguzi dhidi yao.
Akiamuru washukiwa hao wasalie korokoroni hadi Machi 24, 2022, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Milimani Nairobi, Bw Gilbert Shikwe alisema, “Polisi wanahitaji kupewa muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi katika kesi hii iliyo na umuhimu mkubwa kwa umma.”
Bw Shikwe alisema kuibiwa na kudhulumiwa kwa afisa huyo wa Ubalozi wa Zimbabwe kumezua utata katika sekta mbalimbali.
“Uchunguzi wa kina katika kesi hii unahitajika kabla ya washukiwa kufunguliwa mashtaka,” alisema Bw Shikwe.
Bw Shikwe aliagiza washukiwa hao James Mutinda Muema, Samuel Wafula, Muswahili, Charles Omondi Were, Obano, Hassan Farah Forah, Wanjuki Lincoln Kinyanjui, Mbugu, Fundi, Maina, Ngure, Shitekha, Martin Kamau Maina, Shadrack Ambia Luyeku, Shadrack Kioko Nyamai, Cliff Gikobi Oyaro na Joseph Kibui Mukambi wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Gigiri hadi Machi 24, 2022.