Habari Mseto

Wanaosumbua polisi wakati wa kafyu waonywa

April 17th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Rais Uhuru Kenyatta ametoa onyo kwa watu wanaohitilafiana na maafisa wa polisi katika jitihada zao kutekeleza kafyu.

Rais Kenyatta aidha amesema hatua kali kisheria zitachukuliwa kwa wanaotatiza shughuli hiyo.

Kwenye hotuba yake kwa taifa mnamo Alhamisi, kiongozi huyo wa nchi alisema kila mmoja afahamu utaratibu na sheria zilizotolewa na serikali zina madhumuni ya kulinda maisha ya Wakenya.

“Yeyote atakayevunja sheria na kutatiza utendakazi wa maafisa polisi, ataadhibiwa kisheria,” Rais akaonya kupitia hotuba yake iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga kutoka Ikulu jijini Nairobi.

Kafyu ya usiku, kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi na moja za asubuhi inaendelea kutekelezwa kote nchini ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid – 19, unaosababishwa na virusi hatari vya corona. Ilianza kutekelezwa Machi 27, 2020.

Baadhi ya wananchi wanalalamikia inavyotekelezwa, wakinyooshea maafisa wa polisi kidole cha lawama kwa kuwadhulumu. Visa kadhaa vya mauaji na majeruhi yanayohusishwa na utekelezaji wa kafyu vimeripotiwa maeneo tofauti nchini.

Akipongeza utendakazi wa idara ya polisi, Rais Kenyatta hata hivyo amewataka maafisa wa usalama kutekeleza kafyu kwa njia ya utu. “Kwa maafisa ambao wanatulinda usiku na mchana, langu ni kuwapongeza. Pia, mfanye kazi kwa njia ifaayo. Mtekeleze kafyu kwa huruma, muongeleshe anayekosea na mumweleze hatari anayojiwekea yeye mwenyewe na kwa wengine,” Rais akahimiza.

Alisema ni wajibu wa serikali kuhakikisha maisha ya Wakenya yamelindwa dhidi ya janga la Covid – 19.