Makala

'Wanaotaka kura za Mlima Kenya watangaze ni jinsi gani watalifaa eneo'

June 18th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

‘SHIDA’ kuu ya Mlima Kenya katika siasa za urithi wa urais 2022 zimebainika kuwa ndani ya mkataba wa kuahidiwa mgao wa keki ya kitaifa.

Katika hali hiyo, aliyekuwa mwenyekiti wa mpango wa kiusalama wa Nyumba Kumi Joseph Kaguthi anasema sio kwamba watu wa Mlima Kenya hawawezi kufikia uwiana kuhusu mfaafu zaidi mwaka 2022.

“Ni lazima tuahidiwe kuwa hatutaangamizwa na funza wa umaskini tukishapiga kura zetu,” anasema Kaguthi.

Kaguthi anasema kuwa itakuwa hatari kubwa sana kwa Mlima Kenya kujiingiza katika ujinga sawa na wa ndovu ambaye huvamia mabonde, miti na mawe kwa pembe zake bila ufahamu wa thamani halisi ya pembe hizo.

“Ndovu angejua thamani ya hizo pembe zake, hangewahi hata mara moja kufikiria kuvamia kwa hasira akizitumia ovyo. Sawa na sisi wa Mlima Kenya, hatungekuwa na ujinga wa kutumia wingi wetu wa kura kama kifaa cha kulumbana wenyewe kwa wenyewe bali tungekuwa katika meza moja tukijadiliana kuhusu mwelekeo wetu wa umoja,” anasema.

Ni msimamo ambao unaungwa mkono na mrengo mmoja wa baraza la wazee wa Agikuyu ukiongozwa na Bw Peter Munga anayewakilisha Kaunti za Rift Valley.

Serikali ya baada ya Kenyatta

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria anateta kuwa shida kuu ya Mlima Kenya ni kujipanga kuhusu nafasi yake ndani ya serikali hiyo ya baada ya Rais Uhuru Kenyatta.

“Kuna ile hali ya mtu akiwa na bekari ya kutengeneza mikate na ndiyo tuko kwa sasa kama watu wa Mlima Kenya. Tunachumbiwa na wahisani na washirika wa kisiasa kuhusu bekari yetu na mikate. Uamuzi kwa sasa ni aidha tupeane bekari, au mikate au vyote viwili. Mjadala uko hapo,” anasema Kuria.

Anasema kuwa bekari ni kura za ujumla za Mlima Kenya, mkate ukiwa uamuzi wa kupigia kura mwaniaji wa urais.

“Tukipeana bekari kiharamu mambo yaharibike na tujipate kwa mataa ya kisiasa, tutaangamia kwa kuwa hatutakuwa na uwezo wa kujipia mikate…tukiepeana mikate na tubakie na bekari, basi hata kuharibike ndani ya serikali ya urithi huo wa 2022, tutarejelea harakati za kujipikia mikate,” asema.

Anasema kuwa bekari ni “mtu wetu ndani ya serikali hiyo huku mikate ikiwa ni manufaa.”

Katika hali hiyo, Kuria anasema ndio kiini chake cha kuwania urais ili ahifadhi bekari hiyo ndani ya Mlima Kenya.

Hizi ndizo siasa Rais Uhuru Kenyatta anaonekana kupinga akiwasuta wanaoziendeleza kama “takataka na ambao badala ya kufanya kazi ya kuendeleza walikochaguliwa kuwajibikia, wanajihusisha na siasa za ukubwa wa kiserikali.”

Rais anasema kuwa yeye kuna ile barabara ambayo “nimeundia watu wetu na ambayo itakuwa ya kuwafaa wote kutangamana na wote wa taifa hili pasipo ghasia na kubaguliwa.”

Ni katika hali hiyo ambapo wako wanaohisi kwamba hesabu ya Rais pengine iko kwingine nje ya ahadi yake ya 2013 kuwa ataunga mkono naibu wake, William Ruto kurithi mamlaka ya urais.

“Hamtanizuia kufuata barabara ambayo nimejiamulia ya kuwafaa watu wetu (jamii za Mlima Kenya) na nitaifuata kwa dhati. Ukifikiria utapingana na mimi, wewe ngojea uone vile nitakufurusha kutoka hata penye wewe uko kwa sasa. Siasa za baadaye ni za umoja wa kitaifa wala sio umoja wa vyeo na ukubwa… Ni umoja wa kuhakikisha kuwa watu wetu hawatasumbuliqwa na ghasia tena hata baada ya miaka mingine 50,” akasema rais akiwa katika kongamano la dini ya Akorino katika ukumbi wa michezo wa kasarani.

Onyo hilo la Rais linawiana na lingine alilotoa katikati ya mwaka 2018 alipoonya kuwa yeye ndiye sauti ya Mlima Kenya.

“Mkifikiria sitakuwa na neno kuhusu urithi huo, wewe ngojea. Uamuzi wangu utawashtua ninyi wote mnaojihisi kuwa mnaelewa siasa,” alisema Rais Kenyatta.

Ni katika msingi huo ambapo mrengo ambao huunga mkono umoja wa Rais Kenyatta na Raila Odinga ndani ya handisheki unaonya kuwa wanaoendeleza siasa za kumuahidi Ruto kura ni wasaliti wa bekari ya Mlima Kenya na ambapo wanalenga kuichuuza kama kifaa kisicho na manufaa yoyote.

Aliyekuwa Mbunge wa Maragua, Elias Mbau anaonya mrengo unaojiegemeza kwa Ruto dhidi ya kuchuuza kura za Mlima Kenya kama “mitumba bei ya kufunga kazi.”

Bw Mbau ambaye naye huunga mkono mrengo unaofahamika kama Kieleweke na ambao hufikiria kinyume na ule wa Ruto aliteta kuwa wale wote ambao wanaenda kila mahali nchini Kenya wakiahidi kura za wenyeji Mlima Kenya “kama waliopungukiwa na umakinifu kuhusu biashara ya kisiasa.”

Alisema kuwa katika mwaka wa 2022 kura za Mlima Kenya zitakuwa zimegonga 9.2 milioni hivyo basi kuwa tegemeo kuu la wawaniaji wa urais kuzinasa ili waibuke washindi.

“Mbona uwe na mrembo anayemezewa mate na kila mwanamume lakini badala ya ungoje achumbiwe na ushindani uongeze mahari, wewe unamwasilisha kwa boma la mwanamume na kusema umempeana bila hata kuahidiwa mahari?” akawaza.

Mbau anasema Ruto anafaa kuahidi Mlima Kenya mahari yao ni kiasi gani kwa kumpa mrembo wao ambaye ni ukwasi wa kura.