Wanaotapeli kwa jina la mkewe Ruto wasakwa na polisi

Wanaotapeli kwa jina la mkewe Ruto wasakwa na polisi

Na MWANGI MUIRURI

POLISI katika Kaunti ya Murang’a wameanzisha uchunguzi kwenye kisa ambacho wanaume watatu na mwanamke wanadaiwa kuyalaghai makundi ya wanawake Sh1 milioni kwa kutumia jina la Bi Rachel Ruto, mkewe Naibu Rais William Ruto.

Kwenye ukora wao, walaghai hao wamekuwa wakiwashawishi wenyeji kwa kuwaambia kuwa kila mmoja ajisajili kwa ada ya Sh630, wakiahidi kuwa Bi Ruto atazuru kaunti hiyo na kuwapa zawadi za Krismasi zenye thamani ya Sh10,000 kila mmoja Disemba 24.

Kati ya zawadi walioelezwa wanatarajia kupokezwa ni bandali za unga ngano na mahindi, mafuta ya kupikia, mchele na sharubati.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika kambi ya Dkt Ruto, Bw Dennis Itumbi jana Ijumaa alithibitishia Taifa Leo kuwa Bi Ruto hashiriki mpango wowote kama huo wala hajaratibiwa kuzuru Murang’a siku hiyo.

“Sisi hatuwaulizi watu wajisajili kwa pesa kabla ya kuwapa misaada. Masuala yetu yote huendeshwa kwa njia ya uwazi,” akasema Bw Itumbi.

Mshirikishi wa shughli za serikali eneo la Kati, Wilfred Nyagwanga naye alisema kuwa wanaume hao tayari wamekusanya Sh945,000 kutoka kwa wanawake 1,500.

Mkuu wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake (MWO) eneo la Murang’a alisema wanawake waliopunjwa waliweka suala hilo siri kwa kuwa hawakutaka waume wao wagundue.

Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini, Alexander Shikondi alisema ameagiza walaghai hao wakamatwe.Afisa huyo alitoa wito kwa wote ambao wamelaghaiwa fedha zao wafike katika vituo mbalimbali vya polisi kuandikisha taarifa.

“Ni hatia kukusanya pesa kutoka kwa watu ukiwaahidi faida ambazo hazipo. Pia tunalenga waliobuni mpango huo ambao nia yake ilikuwa kuwafilisi watu kwa kutumia jina la Naibu Rais,” akaongeza.

Mshirikishi wa tawi la vijana wa UDA katika Kaunti ya Murang’a, Mixson Warui naye alidai kuwa wanawake ambao wanaratibisha masuala ya makundi hayo ndio walihusika na ukora huo na hawafai kusazwa wakati wa uchunguzi.

“Binafsi nilijuzwa kuhusu suala hilo na mamangu aliponipigia simu nimtumie Sh630 ili ajisajili. Nilishangaa pale aliponiambia watakuwa wakipokezwa zawadi ya Krismasi kutoka kwa Mama Ruto,” akasema Bw Warui.

You can share this post!

Jumwa na wengine 6 wataka kesi ya ufisadi dhidi yao...

Mkufunzi mpya Rangnick hana nia ya kuachilia Man United...

T L