Habari Mseto

Wanaotumia majitaka kufanya kilimo Nairobi waonywa

August 13th, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

GAVANA Mike Sonko ametoa onyo kwa wanaofanya shughuli za kilimo katika Kaunti ya Nairobi kwa kutumia majitaka.

Bw Sonko amesema ukuzaji wa mimea kwa majitaka ni mojawapo wa kiini cha magonjwa kama vile Saratani.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Nairobi, Sonko alisema serikali yake haitafumbia macho wanaofanya kilimo hatari.

Gavana huyo alisema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wakulima Nairobi wakizalisha mazao kwa kutumia majitaka na yenye kemikali.

“Kilimo cha majitaka Nairobi kimevuka mipaka. Chakula kinachozalishwa ndicho tunaletewa sokoni. Mazao ya aina hiyo si salama katika afya zetu na yanachangia pakubwa katika kusababisha magonjwa hatari ikiwemo saratani,” alisema.

Gavana Sonko amedokeza kwamba maafisa wa idara ya kilimo katika Kaunti ya Nairobi kwa ushirikiano na wale wa serikali kuu na halmashauri ya kitaifa ya mazingira (Nema) wataanza msako kukamata wanaokuza mimea kwa kutumia majitaka.

Aidha, alitaja eneo la Njiru kama lililoathirika pakubwa.

Baadhi ya wakulima Nairobi wamekuwa wakizalisha mboga za aina mbalimbali, viazi asili (nduma) na ndizi kwa kutumia majitaka.

Mitaa mingine ambako kilimo kwa kutumia majitaka kimezidi ni Zimmerman, Githurai, Kahawa West na mitaa jirani.

Ni muhimu kutahadharisha kuwa majitaka yana uchafu wa kila aina, kemikali inayotumika kwenye vyoo ikijumuishwa.

Bw Sonko alisisitiza kuwa harakati za kufunga viwanda vinavyoachilia majitaka bila kuyatibu pamoja na wanaoharibu mazingira kiholela Nairobi hazitalegezwa.