Habari Mseto

Wanaotupa maski kiholela waonywa

July 24th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Maski zilizotumika na kutupwa kiholela na kutapakaa kwenye majaa ya taka huenda zikaweka watu katika hatari ya kuambukizwa Covid-19.

Hofu hiyo imeibuka kufuatia barakoa zinazoonekana kutapakaa kwenye dampo na njia za mitaa, isijulikane hali ya watumizi wake.

Dampo la Dandora, Nairobi, limetajwa kama lililoathirika pakubwa.

Ikikiri kufahamu kuwepo kwa utepetevu huo miongoni mwa wananchi, Wizara ya Afya imesema Kenya ina changamoto nyingi za utupaji wa taka.

“Hapa hapa katika Bustani ya Uhuru Park, utaona maski zilizotupwa kiholela zimetapakaa. Kuna shida kubwa nchini namna ya kutupa taka,” akasema Waziri Msaidizi katika Wizara Dkt Mercy Mwangangi Alhamisi katika kikao na wanahabari katika makao Makuu ya Afya, Nairobi, wakati akitoa taarifa ya maambukizi ya Covid-19 nchini.

Aidha, Waziri alisema ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha mazingira ni safi badala ya kuachia jukumu hilo asasi husika kama vile Mamlaka ya Kitaifa Kuhifadhi Mazingira (Nema).

“Tuwajibike na kuhakikisha mazingira yetu ni safi,” Dkt Mwangangi akahimiza, wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kufuatia malalamishi ya maski kutapakaa katika majaa na njia za mitaa.

Suala la utupaji maski kiholela limeibuka wakati ambapo visa vya maambukizi ya Covid-19 vinaendelea kuongezeka kwa kasi.

Mnamo Alhamisi, Kenya iliandikisha idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya corona katika kipindi cha saa 24 zilizopita, baada ya watu 796 kupatikana kuwa na virusi kutoka kwa sampuli 6,754 zilizofanyiwa vipimo, huku wagonjwa watatu wakithibitishwa kufariki.