Habari Mseto

Wanaougua Saratani South Rift kupokea matibabu

April 19th, 2018 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

WAGONJWA wa saratani kutoka kaunti zaidi ya tano eneo la South Rift watapokea matibabu katika hospitali ya Nakuru Level Five kuanzia mwezi Mei.

Kitengo hicho kipya katika hospitali hiyo kinatarajiwa kuwahudumia wagonjwa 30 kwa siku.

Kulingana na msimamizi mkuu wa hospitali hiyo Dkt Joseph Mburu, kitengo hicho kitakuwa na wataalamu wanaoshughulika na magonjwa ya saratani.

“Wagonjwa hao pia watapokea huduma za kisaikolojia ili kuhahakikisha kuwa matibabu wanayoyapata ni kamilifu,” alisema Dkt Mburu.

Alisema kuwa kuna mazungumzo yanayoendelea kuhakikisha kuwa wagonjwa hao wataweza kulipia huduma hizo kwa njia ya National Health Insurance Fund (NHIF).

Katika mazungumzo ya hapo hawali, gavana Lee Kinyanjui alisema kuwa serikali ya kaunti iko katika harakati za kuongezea idadi ya huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.

Hii ni pamoja na kutoa mafunzo  kwa wanafunzi chini ya kitengo cha mafunzo.

Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa kutoka kaunti za Nakuru, Baringo, Nyandarua, Kericho na Samburu.