Habari Mseto

Wanaougua virusi vya corona sasa ni 126

April 4th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe ametangaza kuwa Kenya imeandikia visa nne zaidi vya maambukizi ya virusi vya corona ndani ya muda wa saa 24 zilizopita.

Hiyo inafikisha 126 idadi jumla ya visa hivyo nchini tangu kisa cha kwanza kilipogunduliwa mnamo Machi 12 mwaka huu.

Bw Kagwe alisema miongoni mwa wanne hao, watatu ni Wakenya ilhali mmoja ni raia Pakistan.

“Watu wawili kati yao waliingia nchini hivi majuzi kutokana Malawi na Pakistan na wengine wawili walipata virusi hivyo humu nchini,” akasema Waziri kwenye kikao na wanahabari katika Jumba la Afya, Nairobi Jumamosi alasiri.

Wagonjwa hao wapya wana umri wa kati ya miaka 34 na miaka 44 na watatu ni wanaume huku mmoja akiwa mwanamke.

Waziri Kagwe pia alitangaza kuwa jumla ya watu 1, 781 ambao huenda walitangamana na watu waliambukizwa virusi vya corona pia wanachunguzwa.

Vile vile alitangaza kanuni mpya ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo wa Covid-19 akisema kuwa yoyote anaingia katika maduka ya jumla au masoko ya wazi sharti wavalie barokoa.

Bw Kagwe alisema serikali inaendelea na mpango wake wa kuajiri jumla ya wahudumu wa afya 5,500 akieleza kuwa tayari Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta imewaajiri wahudumu 1,000.

“Zoezi hili linaendeshwa kwa ushirikiana na Bodi za Uajiri wa Watumishi wa Umma katika Serikali za Kaunti nchini,” akasema.

Mnamo Ijumaa idadi ya watu walioambukizwa virusi hivyo ilifika 122 baada ya Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi kutangaza visa vipya 12.

Mtu wa hivi punde kufariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 ni mvulana mwenye umri wa miaka sita ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta akiugua magonjwa mengine sugu.

Jumamosi, Bw Kagwe alikariri kauli ya Waziri wa Biashra na Ustawi wa Kiviwanda Betty Maina kwamba zaidi ya barokoa milioni moja zinatengenezwa na kampuni mbalimbali humu nchini na vitasambazwa kwa wananchi kwa gharama nafuu.

“Baada ya kutengenezwa vifaa hivyo vitapelekwa kwa mawaziri husika wa kaunti ambao watavisambaza kwa wenyeviti wa vyama vya wamiliki wa matatu, bodaboda na tuk tuk kote nchini,” akasema.

“Lakini nawaomba wananchi pia wajinunulie vifaa hivi vinavyotengenezwa humu nchini na mafundi wetu vijana ili nao wafaidike,” Waziri Kagwe akaongeza.