Habari MsetoSiasa

Wanaounga mkono Ruto Pwani waonywa

July 10th, 2018 1 min read

Na KAZUNGU SAMUEL

WABUNGE wawili wa Pwani Jumatatu waliwakosoa wenzao ambao wamekuwa wakimpigia debe naibu wa Rais kuwania Urais mwaka wa 2022.

Wabunge hao, Teddy Mwambire (Ganze) na Omar Mwinyi (Changamwe) walisema kuwa wabunge hao wa ODM ni wasaliti na wakazi wa Pwani wanaangalia kwa makini mienendo yao.

“Hawa ni wabunge ambao ni wasaliti na hivyo mambo yao yako mikononi mwa wakazi wa Pwani ambao ninaamini wanajua vile watakavyowajibu.

Hatuwezi kusema kwamba tunapigania umoja wa Pwani kisha umoja huo ubakie katika watu wachache ambao mienendo yao imekuwa kinyume na matarajio ya wakazi,” akasema Mwambire.

Aidha, mbunge huyo alisema ni mapema mno kwa wabunge waliochaguliwa na chama kingine kuanza kumfanyia kampeni mtu mwingine huku wakitakikana wawe katika msitari wa mbele kuwahudumia wananchi.

“Wabunge hawa ni wasaliti kwa sababu walidanganya wananchi kwamba walikuwa upande huu na wakapewa kura kumbe walikuwa wana malengo tofauti,” akasema Bw Mwambire.

Naye Bw Mwinyi alisema kuwa kwa wabunge hao kuamua kumfuata Bw Ruto kisha kuanza kumpigia debe ni kujitafutia umaarufu wa kisiasa wakati kuna masuala mengi ya kuangalia kwa minajili ya maendeleo ya Wapwani.

“Jambo la kusikitisha ni kuwa hata wakati naibu wa Rais akiwa yuko Pwani kwa ziara ya maendeleo, utawasikia wabunge wenzetu wakianza kusema watamuunga mkono mwaka wa 2022. Hili linashangaza kwamba kufungua barabara na siasa za 2022 ni wapi na wapi,” akahoji Bw Mwinyi.

Aliongeza kwamba idadi ya vijana ambao hawana kazi inaendelea kuwa kubwa katika kaunti ya Mombasa licha ya kuweko kwa raslimali ambazo zingewasaidia wakazi kuimarika kiuchumi.