Michezo

Wanaraga 7 kuimarisha kikosi cha Kabras

July 22nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA wa Enterprise Cup, Kabras Sugar RFC, wamefichua azma ya kujinasia huduma za wanaraga saba pindi muhula wa uhamisho wa wachezaji kwa minajili ya msimu ujao wa 2020-21 utakapofunguliwa.

Kikosi hicho kilicho na makao mjini Kakamega, kilimwajiri kocha mzawa wa Zimbambwe wiki mbili zilizopita kujaza nafasi ya mkufunzi Hennley Du Plessis aliyerejea kwao Afrika Kusini.

Mwenyekiti Philip Jalango ameungama kuwa tayari wamewatambua wanaraga wanaopania kuwasajili kwa matarajio kwamba watawavunia taji la pili la Ligi Kuu ya Kenya Cup msimu ujao.

Hata hivyo, Jalango ambaye amekiri kuwa mchakato wa kuwasajili umeanza, amekataa kufichua majina ya wanaraga hao wanaomezewa na Kabras RFC kwa hofu kwamba kufanya hivyo kutakiuka sera za usajili na pia kutatoa fursa kwa wapinzani wao kuwashawishi vinginevyo.

“Benchi ya kiufundi imekuwa ikiwafuatilia baadhi ya wanaraga wa haiba kubwa tunaohisi kwamba ujio wao utaimarisha makali ya kikosi chetu. Tunalenga kusuka kikosi thabiti kitakachotawala kampeni ya msimu ujao na kutia kapuni mataji mengi iwezekanavyo katika ulingo wa raga ya humu nchini pindi michezo itakaporejelewa,” akasema Jalango.

Jalango amekariri kuwa kocha wa zamani wa Kenya Simbas, Jerome Paarwater ambaye kwa sasa ni mkurugenzi mpya wa raga kambini mwa Kabras RFC, atashirikiana vilivyo na Nyathi kufanikisha kampeni za kikosi hicho msimu ujao.

“Ni wakufunzi wanaojivunia tajriba pevu katika ulingo wa raga na uzoefu huo walio nao utachangia upekee wa Kabras RFC katika raga ya humu nchini na kuinua zaidi viwango vya ushindani na maendeleo ya mchezo huo,” akaongeza Jalango kwa kusisitiza kuwa maandalizi ya Kabras kwa minajili ya msimu ujao yamenoga na usimamizi hukutana mara kwa mara kufanikisha mipangilio mingi ya kikosi.

Hadi shughuli za michezo ziliposimamishwa humu nchini kutokana na janga la corona mnamo Machi 2020, Kabras RFC walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali la Kenya Cup kwa alama 74, tatu zaidi kuliko mabingwa watetezi KCB. Walikuwa ange kutinga fainali kwa mara nyingine baada ya kupangiwa kukutana na mshindi kati ya Impala Saracens na Mwamba RFC kwenye nusu-fainali.

Wanabenki wa KCB walikuwa wakutane na mshindi wa mchujo mwingine kati ya Homeboyz na Menengai Oilers.

Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilifutilia mbali msimu mzima wa 2019-20 kabla ya kupiga abautani na kuuahirisha tu msimu huo baada ya malalamishi kutoka kwa vikosi na washikadau mbalimbali wa mchezo huo humu nchini.

KRU kwa sasa inasubiri mwongozo wa serikali kupitia Wizara ya Michezo kuhusu taratibu zitakazoongoza kurejelewa kwa spoti za humu nchini kabla ya kuchukua maamuzi mengine.