Wanaraga wa KCB watolewa jasho wakipiga Strathmore Leos ligi ya Kenya Cup

Wanaraga wa KCB watolewa jasho wakipiga Strathmore Leos ligi ya Kenya Cup

Na GEOFFREY ANENE

VIONGOZI KCB RFC walizoa ushindi wa saba mfululizo kwenye Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya Cup) baada ya kuzima Leos ya Chuo Kikuu cha Strathmore uwanjani KCB Ruaraka, Jumamosi.

Vijana wa kocha Curtis Olago hawakupata ushindi huo kwa urahisi. Walitolewa kijasho kabla ya kuponyoka na ushindi huo.

Mabingwa hao wa zamani waliongoza 14-0 kupitia miguso miwili na mikwaju yake ikiwemo kutoka kwa Darwin Mukidza.

Leos walipunguza mwanya huo hadi 14-5 kupitia kwa Brunson Madigu kabla ya mapumziko. Madigu aliongeza penalti mbili zilizokata uongozi huo zaidi hadi 14-11.

Leos walichukua uongozi 14-18 walipopata mguso na mkwaju, lakini wanabenki wa KCB wakajibu na dozi sawa kupitia mguso wa Brian Wahinya na mkwaju kutoka kwa Mukidza.

Wanabenki Isaac Njoroge na Johnstone Olindi waliongeza mguso mmoja kila mmoja naye Mukidza akahitimisha kwa mkwaju. Naibu kocha wa KCB, Dennis Mwanja alisifu timu yake kwa kutoachilia mechi hiyo iwaponyoke.

“Tulifanya makosa kadhaa katika kipindi cha pili ikiwemo kushika mipira vibaya, lakini nashukuru vijana walipigana kufa-kupona na kuvuna ushindi,” alisema Mwanja baada ya mchuano huo uliomkumbuka mwendazake Jerry Olola aliyechezea klabu zote mbili.

Mechi ijayo ya KCB ni dhidi ya Monks ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA).

Katika mechi zingine zilizosakatwa Jumamosi, mabingwa watetezi Kabras Sugar walilipua Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta 67-3, Menengai Oilers wakapepeta Mwamba 53-15, Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi wakachapwa 37-8 na Nakuru nao Kenya Harlequin wakanyamazisha Homeboyz 28-11.

Monks walihakikisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro wanasali bila ushindi walipowakung’uta 20-13.

  • Tags

You can share this post!

Maswali chungu nzima baada ya vigogo wa Azimio kususia...

Wahadhiri wapongezwa huku wakiahidi kuendelea kuweka MKU...

T L