Michezo

Wanaraga wa Morans kujifua ili kujiweka fiti

September 25th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Kenya cha raga ya daraja la pili kwa wachezaji saba kila upande almaarufu Morans kimepangiwa kushiriki michuano mbalimbali ya vipute visivyo rasmi msimu ujao.

Haya ni kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), Oduor Gangla ambaye amekariri kwamba vipute hivyo vitatoa jukwaa mwafaka kwa wanaraga wa Kenya kujipima nguvu kadri wanavyojiandaa kwa mapambano mbalimbali ya haiba kubwa yaliyopo mbele yao.

Kati ya vipute ambavyo Morans wanatazamiwa kushiriki ni Dubai Invitational, Roma Sevens, Singapore Invitational a Sudamerica Sevens kitakachoandaliwa nchini Argentina.

Gangla anasema kuwa inasikitisha kwamba kivumbi cha pekee ambacho wanaraga wa Morans hushiriki kwa sasa ni cha Safari Sevens pekee ambacho kwa mujibu wake, hakitoshi kabisa kuwapa ujuzi wa kukabiliana na wapinzani walio na tajriba pevu na uwezo mkubwa katika raga ya kimataifa kila wanapojumuishwa katika kikosi cha Shujaa.

“Wachezaji wa Morans huwa na wakati mgumu sana wanapopangwa katika kikosi cha kitaifa cha wachezaji saba kila upande, Shujaa. Itakuwa vyema zaidi iwapo wataanza kushiriki michuano tofauti ya kirafiki katika ulingo wa kimataifa ili wapate ujuzi na uzoefu utakaowaaminisha zaidi katika siku za halafu,” akasema Gangla huku akisisitiza ukubwa wa matumaini yake kwa kikosi cha Shujaa ambacho kwa sasa kinanolewa na mkufunzi mpya, Paul Feeney.

Hii ni sehemu ya mikakati ya Shujaa ambao kwa sasa wanajiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Olimpiki za 2020 jijini Tokyo, Japan na duru za Raga ya Dunia.

“Baadhi ya wachezaji walianza kujifua kwa michuano hii mnamo Agosti. Ujio wa Feeney, kuundwa kwa benchi nzuri zaidi ya kiufundi na kupatikana kwa mdhamini mpya ni kati ya mambo ambayo naamini yatawapa Shujaa kila sababu ya kutamba katika kampeni zijazo,” akaongeza kinara huyo.

Kufuzu Olimpiki

Mechi za kufuzu kwa Olimpiki zimepangiwa kupigwa mnamo Novemba jijini Johanesburg, Afrika Kusini na kikosi cha Kenya Sevens kwa upande wa wanaume kitatumia michuano ijayo ya Safari Sevens kujiandalia kwa mapambano hayo. Kibarua cha kufuzu kwa upande wa wanawake kimeratibiwa kutandazwa nchini Tunisia mwezi ujao.

Kwingineko, Nondies wamemchagua upya Auka Gacheo kuwa mwenyekiti wao kwa muhula mwingine huku Arune Hicks akihifadhi pia wadhifa wake wa katibu wa klabu.

Katika uchaguzi wao wa hivi karibuni, Nondies walibuni pia nafasi ya meneja wa klabu ambayo ilitwaliwa na Kevin Were. Kikosi hicho kiliimarika sana katika kampeni za Ligi Kuu ya Kenya Cup msimu huu huku wakiorodheshwa wa sita katika Raga ya Kitaifa ya Sevens iliyowashuhudia wakijizolea jumla ya alama 68.