Michezo

Wanariadha kuanzisha mbio mpya North Rift

April 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA mara mbili wa marathon katika Riadha za Dunia, Abel Kirui na mshindi wa Barcelona Half Marathon, Victor Chumo, wamefichua mpango wa kuasisi mbio za kilomita 45 ziitwazo Patriotic Road Run.

Baadaye mwaka ujao, mbio hizo zitaanza kushirikisha wanariadha maarufu na chipukizi kutoka kaunti tatu za eneo la North Rift – Nandi, Uasin Gishu na Elgeyo Marakwet kwa minajili ya maendeleo ya jamii.

Kwa mujibu wa Kirui, makala ya kwanza ya riadha hizo mwaka huu yataandaliwa katika kipindi cha wiki chache zijazo na zitawashirikisha wao wawili pekee.

Amekiri kwamba kwa sasa wanatafuta kibali kutoka kitengo cha Kitaifa cha Huduma kwa Polisi na Wizara ya Afya ili kufanikisha matayarisho ya mashindano hayo yatakayowapa jukwaa mwafaka la kuchangisha fedha kwa minajili ya kukabiliana na janga la virusi vya corona.

Kubwa zaidi linalowaaminisha kuwa ombi lao litakubaliwa, ni kwamba mbio za mwaka huu hazitakiuka kanuni mpya ya sasa ya serikali inayoharamisha mikusanyiko ya umma kwa kuwa washiriki ni wawili tu.

“Naamini tutafaulu kuandaa makala ya kwanza chini ya wiki chache zijazo. Tutapania kudumisha umbali wa hadi mita 10 baina yetu, jambo ambalo litakuwa rahisi kwa kuwa tutakuwa wawili katika mashindano yenyewe,” akaongeza Kirui kwa kusisitiza kwamba wataanza mbio hizo katika Kaunti ya Nandi, kupitia Uasin Gishu na kumalizia Elgeyo-Marakwet.

Kirui aliyeibuka mshindi wa nishani ya fedha katika marathon ya Olimpiki za 2012 jijini London, Uingereza; anashikilia kwamaba kushiriki kwao mbio za Patriotic Road Run kutawapa fursa ya kujifua vilivyo kwa Prague Half Marathon ambayo imeahirishwa hadi Agosti 2020. Awali, mbio hizo zilikuwa zifanyike Aprili katika Jamhuri ya Czech.

“Tuko katika hatua za mwisho za maandalizi. Riadha hizi mpya zitapiga jeki juhudi za kukabiliana na corona, zitatuwezesha kujinoa ipasavyo na pia kuhamasisha wanariadha wengi kutoka maeneo haya ambayo ni ngome za watimkaji wa haiba kubwa duniani,” akaongeza Kirui aliyeshinda pia medali ya shaba katika Rotterdam Marathon mnamo 2009.

Mbali na kushikilia ufalme wa mbio za Chicago Marathon na Vienna Marathon, Kirui anajivunia pia kutawala mbio za Berlin Marathon mnamo 2009 kisha Daegu Marathon mnamo 2011.

“Tumekuwa tukishiriki vipindi viwili vya mazoezi ya kilomita 30 kila jioni. Sasa tunapanga kuanza kukimbia umbali wa kilomita 20 kila asubuhi,” akasema Kirui huku akitaka serikali kuwafanyia wanariadha wote wa humu nchini vipimo vya afya, ili wale watakaokosa kupatikana na virusi vya corona waruhusiwe kuendelea na mazoezi katika zaidi ya kambi 60 za mbio zilizoko Nandi, Uasin Gishu na Elgeyo Marakwet.

Mbali na Riadha za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 zilizokuwa zifanyike jijini Nairobi kati ya Julai 7-12, mashindano mengineyo ambayo yameahirishwa kwa sababu ya corona ni ya Indoor Championships mjini Nanjing, China; Nusu Marathon ya Dunia mjini Gdynia, Poland na Matembezi ya Dunia yaliyokuwa yaandaliwe mjini Minsk, Belarus.

Kufikia sasa, mamia ya wanariadha wa humu nchini tayari wamekiri kukadiria hasara tangu kusimamishwa kwa shughuli zote za michezo hadi janga la corona litakapodhibitiwa vilivyo.