Michezo

Wanariadha wapokea msaada kutoka kwa Athletics Kenya

June 9th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ZAIDI ya wanariadha 1,000 kutoka Kaunti za Makueni na Machakos wamepokea msaada wa chakula kutoka kwa Chama cha Riadha cha Kenya (AK).

Makamu Rais wa AK, Paul Mutwii, amesema wameweka mikakati maalumu kuhakikisha kwamba hakuna mwanariadha yeyote atakayeathirika kutokana na janga la corona.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa AK Tawi la Nairobi, Barnaba Korir aliyetoa pia vifaa vya wanariadha kujikinga dhidi ya ugonjwa wa corona.

Wengi wa wanariadha hao walitarajiwa kuwakilisha Kenya katika mashindano ya dunia ya watimkaji wasiozidi umri wa miaka 20 uwanjani Kasarani mwezi ujao.

Mashindano hayo yaliahirishwa kutokana na ugonjwa wa Covid-19. Mutwii ameshikilia kwamba misaada yote kwa wanariadha wa humu nchini ni sharti ipitie kwa chama cha AK ili iwafikie wanariadha wanaostahili kusaidiwa.

Aidha, zaidi ya wanariadha wengine 1,400 wamekuwa kambini katika maeneo mbalimbali ya jamhuri huku watakaonufaika katika awamu ijayo wakiwa wale wa Nyahururu na Eastleigh katika Kaunti za Laikipia na Nairobi mtawalia.