Makala

Wanasiasa serikalini wanaomiliki baa wanavyotishia polisi    

April 10th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MAAFISA wa polisi eneo la Mlima Kenya sasa wanaitaka serikali kutoa marufuku ya kumiliki baa dhidi ya wanasiasa walio mamlakani.

Polisi wamesema kwamba wanasiasa hao huungana kuchochea adhabu dhidi ya maafisa wanaotekeleza kazi kudumisha sheria.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu kiusalama eneo la Kati alidokezea Taifa Dijitali kwamba “huku tuna zaidi ya wanasiasa 65 ambao wanamiliki baa”.

Alisema kwamba wanasiasa hao sanasana wako katika mabunge ya kaunti, na ni nyapara wa serikali zizo hizo zinazojukumika kutoa leseni.

“Wanasiasa hao huhakikisha kwamba wamepata leseni za baa zao, wametumia ushawishi wao wa kisiasa kukiuka sheria na pia kuadhibiwa kwa maafisa watakaovamia baa zao,” akasema.

Murang’a imetajwa kama mojawapo ya kaunti ambapo mwanasiasa mwenye wadhifa mkuu serikalini, katika familia yake kuna wamiliki 23 wa biashara ya uuzaji vileo.

“Vilabu vyao vyote hata vile vilivyo karibu na shule na vyenye historia ya kuuza pombe hatari, vinapata leseni kwa sababu ya ushawishi wake,” akasema.

Polisi anayeshinikiza sheria ifuatwe kikamilifu, hutishiwa kuhamishwa au hata kufutwa kazi.

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye anaongoza vita dhidi ya pombe haramu na hatari, sasa anatakiwa kuhakikisha kwamba hata wanasiasa wawekezaji wa biashara za mivinyo wamedhibitiwa.

“Wanasiasa ndio hatari zaidi katika uuzaji mvinyo. Mji wa Murang’a, kwa mfano, kuna wanasiasa kadha ambao wanaongoza mtandao wa biashara ya uuzaji pombe ambazo hazijaafikia ubora,” akasema afisa mmoja wa kiusalama Murang’a Mashariki.

Aliongeza kwamba “huwezi ukaandama mtandao huo wa wanasiasa kisheria kwa kuwa wao hukutisha na kuandaa maandamano”.

Baa zinazomilikiwa na washirika wa wanasiasa hao hukiuka sheria, ikiwemo, saa za kuhudumu.

Isitoshe, vituo vyao kelele za miziki ya juu huwa zimesheheni.

Afisa huyo alisema kwamba wanasiasa hao huficha pombe haramu ndani ya nyumba zao na kwa kuwa wameungana na kuwa na mizizi ya kisiasa na hata ndani ya usalama, wao ni serikali, Katiba na sheria kivyao.

Alidai kwamba kila afisa ambaye hutumwa kufanya kazi ni lazima kwanza afahamu mitandao hiyo ya kisiasa na ambapo onyo hutolewa kuhusu kutatiza mpangilio wa kibiashara.

Maafisa kadha wameripoti kuhamishwa kupitia ushawishi wa wanasiasa na washirika wao wa biashara ya mivinyo.
[email protected]