WANDERI KAMAU: Wanasiasa wakome kudhalilisha IEBC hadharani, wanaweza kuzua ghasia

WANDERI KAMAU: Wanasiasa wakome kudhalilisha IEBC hadharani, wanaweza kuzua ghasia

Na WANDERI KAMAU

UCHAGUZI Mkuu wa 2022 unaponukia, macho yote sasa yanaelekezwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kati ya makundi yanayofuatilia utendakazi wake kwa karibu ni wanasiasa, Wakenya na jamii ya kimataifa.Mwenendo wa tume hiyo ndio utakaoamua ikiwa Kenya itaendelea kuwa mfano wa nchi za kuigwa barani Afrika, ama itatumbukia tena kwenye giza lililoikumba baada ya uchaguzi wenye utata wa 2007.

Kwa mantiki hiyo, huu ni wakati muhimu sana kwa tume hiyp kupewa nafasi kuendesha shughuli zake bila kuingiliwa kwa namna yoyote ile. Urejeleo huu unatokana na kauli za baadhi ya wanasiasa kwamba, baadhi ya makamishna wake wamegawanyika kwa misingi tofauti ya kisiasa.

Kwa mfano, baadhi ya wanasiasa wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, wanamlaumu mwenyekiti wake, Wafula Chebukati, kwa “kuupendelea” mrengo wa Naibu Rais William Ruto.

Hii ni baada ya Katibu Mkuu wa UDA, Bi Veronicah Maina, kuiandikia barua tume hiyo, akilalamikia hatua ya baadhi ya mawaziri kujihusisha kwenye siasa.Baadhi ya mawaziri wanaolaumiwa ni Dkt Fred Matiang’i, Joe Mucheru , Eugene Wamalwa kati ya wengine.

Ingawa mawaziri hao wamekanusha madai ya kumpigia debe Bw Odinga kuwania urais mwaka ujao, wanasiasa kamwe hawafai kuiingiza tume hiyo kwenye majibizano yao.Kabla ya ghasia za 2007 kutokea, mirengo ya kisiasa ya ODM (uliomuunga mkono Bw Odinga) na PNU (uliomuunga mkono Rais Mstaafu Mwai Kibaki) ilijibizana vikali kuhusu ikiwa Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK) ingeendesha uchaguzi huo kwa njia huru na ya haki.

Majibizano hayo yalizaa taharuki ambayo matokeo yake yalikuwa ni mrengo mmoja kudai kulikuwa na wizi wa kura na hatimaye machafuko ambayo hayakuwa yamewahi kushuhudiwa nchini kutokea.

 

akamau@ke.nationmedia.com

You can share this post!

Viongozi wa kidini wakosoa wanasiasa kuhusu kampeni za...

Atiwa mbaroni korti ikidumisha Ringera

T L