TAHARIRI: Aibu wanasiasa kumwaga pesa njaa ikikeketa

TAHARIRI: Aibu wanasiasa kumwaga pesa njaa ikikeketa

Na MHARIRI

MATUKIO ya wanasiasa yanayoshuhudiwa nchini yamekuwa yakiwashangaza wananchi wengi hasa namna ambavyo kampeni hizo zilianzishwa mapema huku serikali iliyo mamlakana ikiendelea kujikokota kutimiza ahadi zake kwa Wakenya.

La kushangaza zaidi ni namna ambavyo baadhi yao wanatumia mamilioni ya pesa kuandaa kampeni hizo kubwa kubwa na hata kumwaga pesa kwa wanaohudhuria mikutano hiyo bila kujali mahangaiko chungu nzima yanayoendelea kuwazonga wananchi wa kawaida kuu likiwa ni janga la njaa.

Kufikia sasa, takwaimu rasmi zinaonyesha kwamba zaidi ya Wakenya 2.5 milioni wanakabiliwa na baa la njaa katika kaunti zipatao kumi na mbili.

Hali hii huenda ikawa mbaya zaidi ikizingatiwa kuwa kiangazi kinaendelea kukumba maeneo mengi huku mvua inayotarajiwa ikiendelea kukawia kufikia sasa.

Mbali na janga la njaa, wafugaji wanaendelea kuatilika kwa hasara kufuatia kuangamia kwa mifugo yao wanaoitengemea pakubwa kutokana na ukosefu wa malisho na maji.

Vivyo hivyo, hali hii ya kiangazi inaendelea kukithiri hasa maeneo ya Marsabit, Isiolo, Baringo na Turkana.

Ni kinaya habari kuibuka kwamba kuna maeneo nchini ambapo chakula kimefurika huku sehemu zingine zikiumia kwa ukosefu wa mlo.

Maeneo ya Trans Nzoia na Uasin Gishu yanadaiwa kuwa na zao la mahindi kwa wingi na wakulima wanaendelea kusaka soko la zao hilo.

Ni katika mazingira haya ambapo viongozi wengi wanaonekana wazi kupuuza kilio cha mwananchi ya chini huku wakijifanya wakombozi wao katika uongozi wa serikali ijao baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Swali kuu ni je, wanaoomba kura hawaoni wananchi wa kawaida akiumia kutokana na baa la njaa?

Kisa cha hivi majuzi ambapo wanabodaboda na mama mboga walikuwa wakipigania pesa kutoka kwa mwanasiasa wa humu nchini ni ushahidi tosha kwamba wanasiasa hawa wanaendesha kampeni zao kwa kutumia mamilioni ya mifedha na wameamua kupuuza kilio cha mwananchi wa chini ili kwanza waweze kumpumbaza ampe kura mwaka 2022 ndipo baadaye amtelekeze kama ilivyo ada katika ulingo wa siasa za nchi hii.

Ni fedheha kubwa kwa wanasiasa na viongozi hawa ambao wanaendesha unyama huu kwa kujali ubinafsi wao wa kujitimizia matakwa yao bila kujali chochote kuhusiana na maisha wa wanadamu.

Wakati umefika wa wananchi kuwapiga darubini ili kuwachuja katika uchaguzi mkuu ujao la sivyo maisha wa Mkenya itasalia kuwa ya umasikini miaka nenda miaka rudi.

You can share this post!

Boda atupwa nje kwa kutafuna muguka huku ibada ikiendelea

Mchujo wamtia Raila baridi

T L