Wanasiasa wanaofadhili ghasia Kapedo kukamatwa

Wanasiasa wanaofadhili ghasia Kapedo kukamatwa

JOSEPH OPENDA na VALENTINE OBARA

WAZIRI wa Usalama Fred Matiang’i, amesema polisi wanachunguza wanasiasa kadhaa wanaoshukiwa kufadhili ghasia katika eneo la Kapedo kwenye mpaka wa kaunti za Turkana na Baringo.

Akizungumza jana jijini Nairobi, Dkt Matiang’i alisema vita vya mara kwa mara eneo hilo vimegharimu nchi rasilimali nyingina maafa.

“Kuna utamaduni wa kulinda wahalifu ikidaiwa wanatekeleza desturi ya wizi wa mifugo. Ukweli ni kwamba hivyo vita hufadhiliwa kisiasa na kuna watu tunaowaandama wakiwemo viongozi. Tutachukua hatua kali kuhakikisha wote wanaohusika wameadhibiwa,” akasema.

Alitoa kauli hiyo baada ya kamanda wa kikosi cha polisi wa GSU kuuawa na majangili wikendi katika eneo la Ameyen, karibu na Kapedo.

Dkt Matiang’i alisema watafanya oparesheni kali katika eneo hilo.

“Tutakapomaliza oparesheni yetu, itakumbukwa kwa miaka mingi,” akasema.

Katika shambulio hilo lililosababisha wabunge watatu na wanahabari kukwama Kapedo wakihofia usalama wao, polisi wengine watatu walijeruhiwa.

Kamishna wa eneo la Rift Valley, George Natembeya, alisema hapakuwa na sababu yoyote ya majangili hao kushambulia polisi ambao walikuwa katika ziara ya kutafuta eneo la kujenga kambi mpya ya GSU.

“Tumepoteza maafisa wawili katika muda wa wiki mbili. Majangili hao wamevuka mpaka. Tutahakikisha sheria inadumishwa,” akasema Bw Natembeya.

Mmoja wa maafisa waliojeruhiwa amelazwa katika hospitali ya Mediheal mjini Nakuru na wengine wawili walisafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu maalum.

You can share this post!

K’Osewe alidai nilichovya asali ya mkewe, mshtakiwa...

Waganda washerehekea kurejeshwa kwa intaneti