Wanasiasa wang’ang’ania mahasla

Wanasiasa wang’ang’ania mahasla

Na BENSON MATHEKA

WAGOMBEAJI wakuu wa urais, Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wamebuni mbinu za kuwavutia vijana na Wakenya wa mapato ya chini wakiahidi kuwasaidia wakishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Hii ni baada ya kutambua kuwa hakuna anayeweza kushinda urais bila kuungwa mkono na mamilioni ya vijana ambao wengi wao wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha licha ya kuwa nguzo ya uchumi wa nchi.

Dkt Ruto na Bw Odinga, wamebuni kampeni za kuwavutia vijana, wanabodaboda na wachuuzi kila mmoja akiwaahidi minofu iwapo atashinda uchaguzi mkuu wa 2022.

Kupitia kampeni yake ya hasla, Dkt Ruto amekuwa akiahidi kuinua hali ya kiuchumi ya Wakenya wa matabaka ya chini na amekuwa akisaidia makundi ya wachuuzi, wanabodaboda, wauzaji mboga na makanisa.

Ingawa amekuwa akikosoa kampeni ya Dkt Ruto akimlaumu kwa kuhonga watu wa matabaka ya chini ili kuzua vita vya matabaka, Bw Odinga naye anasema atawasaidia vijana kujiinua kiuchumi.

Amebuni kauli mbiu ya Azimio la Umoja ambalo anatumia kukabili kampeni ya hasla ya Dkt Ruto kwa kukutana na wananchi maeneo ya mashinani kuwaeleza mipango aliyo nayo kwa kila eneo.

Waziri mkuu huyo wa zamani anasema kwamba ataanzisha hazina ya wanabodaboda na kuhakikisha pikipiki zinatengezewa humu nchini ili ziwe nafuu kwa vijana wapatao 2.4 milioni wanaozitumia kujipatia riziki.

Kupitia kampeni zao Dkt Ruto na Bw Odinga wamebuni mipango ya kiuchumi wanayolenga kutumia kushawishi vijana ambao ni asilimia 75 ya raia wote nchini.

“Mpango wa uchumi wa kuanzia matabaka ya chini unanuia kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa pesa kwa mamilioni ya Wakenya wasio na ajira, makundi ya biashara za mahasla na wakulima,” asema Dkt Ruto.

Wachanganuzi wa siasa na uchumi wanasema hii ni kwa sababu wapigakura wengi ni vijana ambao wamesoma na hawana kazi au shughuli rasmi za kujikuza kiuchumi.

Wawili hao wamekuwa wakikutana na makundi ya raia wa matabaka ya chini katika juhudi za kuuza sera zao.

“Wanachofanya wagombeaji wakuu wa urais ni kutumia hali ya kiuchumi inayokabili Wakenya, wengi wakiwa vijana ili kuwashawishi kuwaunga mkono na kuwapigia kura kwenye uchaguzi mkuu ujao. Asilimia 75 ya Wakenya ni vijana kumaanisha kuwa ndio wapigakura wengi,” asema mtaalamu wa masuala ya siasa na usimamizo Dorothy Kendi.

Kulingana na mwanaharakati Ndungu Wainaina, kampeni za kuinua masikini kiuchumi za Dkt Ruto na Bw Odinga zinanuiwa kuimarisha kampeni zao.

“Kufikia Oktoba na Novemba Raila Odinga na William Ruto watakuwa na mirengo miwili ya kisiasa. Raila atakuwa na Azimio La Umoja ambalo ataungwa na vyama kadhaa. Ruto atakuwa na mpango wake uchumi wa hasla kuanzia mashinani,” asema Bw Wainaina.

Katika mipango yake kuhusu vijana, Bw Odinga anashikilia kuwa vijana wanaoanzisha biashara wapatiwe likizo ya ushuru ili waweze kujijenga sawa na ilivyopendekezwa kwenye Mswada wa marekebisho ya katiba wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Dkt Ruto alikuwa amepinga mswada huo akisema ulinuia kubuni nyadhifa za uongozi kwa viongozi wachache wa kisiasa na kupuuza maslahi ya wale wa matabaka ya chini.Huku Dkt Ruto akisema ana mikakati ya kuinua hali ya kiuchumi ya Wakenya wa matabaka ya chini, Bw Odinga anasema sera yake inaangazia kukuza uchumi wa maeneo ya mashambani ambako Wakenya wengi wa matabaka ya chini wanaishi.

“Kubadilisha Kenya kutoka nchi masikini hadi yenye ustawi kunahitaji sera zinazolenga kuimarisha utajiri maeneo ya mashambani,” Bw Odinga amekuwa akisisitiza.

Wachanganuzi wanasema kuwa vigogo hao wawili wanaogombea urais wanasema kitu kimoja tu, kwamba wanapigania kura za walalahoi walio wengi nchini.

“Wote wanasema kitu kimoja kwa lugha tofauti. Ukweli ni kwamba wang’ang’ania kura za masikini. Lengo lao ni kushinda kura na sidhani kuna aliye na nia safi au mipango kabambe ya kuinua hali ya maisha ya raia,” aeleza Bi Kendi.

Kwenye taarifa aliyotoa Jumapili, Bw Odinga alisema ananuia kushughulikia masuala ya vijana kupitia sera zinazobuni ajira, kuweka rekodi za vijana walio na ujuzi na kuwawezesha kupata pesa za kuanzisha biashara kwa urahisi.

Mbali na kubuni Hazina ya Taifa ya Bodaboda na viwanda vya kutengeneza pikipiki, Bw Odinga anasema kuwa serikali yake itabuni wizara na tume za kushughulikia vijana pamoja na kuhakikisha wanapata tenda za serikali.

Kwa upande wake, Dkt Ruto anasisitiza kuwa mpango wa kukuza uchumi kuanzia juu umekuwa ukitenga masikini kwa kuwa unawanyima nafasi za kustawi na serikali yake itaweka mikakati ya kujenga uchumi kuanzia chini kwa kuwawezesha vijana kupata kazi na kuimarisha mazingira ya kufanya biashara.

You can share this post!

Njaa: Serikali kuanza kusambaza mlo, maji

Real Madrid wazamisha Valencia na kutua kileleni mwa La Liga