Habari MsetoSiasa

Wanasiasa waonywa wasitumie corona kujinufaisha kisiasa

April 12th, 2020 1 min read

Na TITUS OMINDE

JUMAPILI ya Pasaka iliadhimishwa Jumapili bila shamrashamra zozote huku viongozi wa kidini wakipeperusha mahubiri yao kupitia mitandao, televisheni na redioni.

Katika eneo la North Rift, viongozi wa kidini walitumia ibada za Jumapili ya Pasaka kuonya wanasiasa dhidi ya kutumia janga la virusi vya corona kujinufaisha kisiasa na kuendeleza ufisadi nchini.

Wito sawa na huu ulitolewa katika ibada nyingine zilizopeperushwa kutoka pembe tofauti za nchi.

Viongozi hao walijuta kwamba wanasiasa wanatumia janga hili kujinufaisha kibinafsi.

Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Jimbo Katoliki la Eldoret Dominic Kimengich, alitaka afisi ya Mkurugenzi wa DCI na afisi ya DPP wawe macho kuhakikisha ufisadi hauendelezwi wakati huu.

Askofu Kimengich alisema kuna wanasiasa na Wakenya fisadi ambao wamechukua fursa ya hali hiyo kuendeleza shughuli zao za ufisadi nchini.

“Ni aibu kwa viongozi kutumia Wakenya walio katika mazingira magumu kujipatia umaarufu wa kisiasa,” Askofu Kimengich alisema.

Akihutubia waandishi wa habari baada ya ibada yake ya Jumapili ya Pasaka kupitia kituo cha redio Katoliki cha Upendo mjini Eldoret, aksofu huyo alisifu juhudi zinazowekwa katika vita dhidi ya janga la ugonjwa huo.

“Hakuna kiongozi anayepaswa kutumia hali ya sasa kwa masilahi yake ya ubinafsi. Badala yake wanapaswa kuzingatia ustawi wa Wakenya wanaoumia kutokana na janga la corona,” alisema Askofu Kimengich.

Askofu huyo aliwaambia wananchi watazame kwa makini mienendo ya viongozi wao wakati huu ili wawaweke katika mizani uchaguzi ujao utakapofika.

“Ninaamini Wakenya wanaangalia viongozi kama hao na hawapaswi kuwachagua katika siku zijazo,” aliongeza

Maoni yake yaliungwa mkono viongozi wengine wa kidini ambao ni pamoja na Lincolin Biwott wa Dayosisi ya St Mathews ACK Eldoret, na Askofu John Kamau Mark wa KAG, Langas.

Makasisi hao waliendesha ibada zao kupitia Facebook, WhatsApp na aina nyingine za mitandao ya kijamii kwa kukumbatia Teknolojia ya Mawasiliano na Habari (ICT).