Wanasiasa watoroka mazishi ya Chidzuga kwa kuzuiwa kupiga siasa

Wanasiasa watoroka mazishi ya Chidzuga kwa kuzuiwa kupiga siasa

Na SIAGO CECE

KIZAAZAA kilitokea kwenye mazishi ya aliyekuwa mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kwale, Zainab Chidzuga wakati Gavana Salim Mvurya alipowaongoza wanasiasa kuondoka kwa hasira baada ya kunyimwa fursa ya kuwahutubia waombolezaji.

Familia hiyo kupitia msemaji wake, aliyekuwa Waziri wa Usafiri Chirau Ali Mwakwere, ilikuwa imetoa agizo Ijumaa asubuhi kwamba hakuna mwanasiasa angeruhusiwa kuhutubia waombolezaji.

Kisanga kilizuka wakati kitindamimba wa marehemu Chidzuga, Mariam Chidzuga, alipomuomba Bw Mwakwere amruhusu Katibu wa Wizara ya Kilimo, Hamadi Boga kuzungumza wakati wa mazishi.

Bw Mwakwere badala yake alichukua maikrofoni kutoka kwake na kusisitiza kwamba walikuwa wamekubaliana awali na wanasiasa wote kwamba hakuna yule ambaye angeruhusiwa kuzungumza.

“Ikiwa uko hapa kuzungumza siasa unaweza kuondoka. Iwapo unaomboleza na familia, unaweza kukaa,” alisema.

Jambo hilo lilisababisha wanasiasa waliokuwa wamesalia wakiwemo Waziri Msaidizi katika Wizara ya Ardhi Gideon Mung’aro, Katibu wa Wizara ya Kilimo Profesa Omar Boga, Seneta wa Kwale Issa Boy, Mbunge wa Lungalunga Khatib Mwashetani, Mbunge wa Kinango Benjamin Tayari na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi Jenerali Samson Mwathethe, kuondoka katika hafla hiyo.

Walifuatwa na nusu ya waombolezaji ambao vilevile walipinga uamuzi wa kutowaruhusu wanasiasa kuzungumza.

Haya yalijiri hata baada ya binti ya Bi Chidzuga kumsihi Bw Mwakwere kumruhusu Bw Boga kuhutubia umma.

“Tulikuwa tayari tumejadiliana na wansasiasa kwamba hawatazungumza,” alisema Bw Mwakwere.

Marehemu Chidzuga alizikwa Ijumaa adhuhuri nyumbani kwake Golini, eneo la Matuga, baada ya mwili wake kuwasili katika Uwanja wa Ndege kutoka Nairobi.

Aliaga dunia Alhamisi asubuhi akiwa na umri wa miaka 65, katika Reliance Hospital, Nairobi kutokana na matatizo ya Covid-19.

Bintiye, Mwanaisha Chidzuga, alisema marehemu alikuwa ameugua Covid-19 na akapona lakini akapata matatizo na kulazwa hospitalini.Wachanganuzi walisema mambo yalivurugika baada ya karibu viongozi watano wanaomezea mate kiti cha Gavana Mvurya, kuhudhuria hafla hiyo.

“Walikuwa wamegeuza mazishi kuwa uwanja wa siasa hivyo basi kumruhusu kiongozi mmoja kuzungumza kungechochea joto la kisiasa miongoni mwa waombolezaji,” alisema mwombolezaji mmoja ambaye hakutaka kutajwa.

Rais Uhuru Kenyatta, kupitia hotuba iliyosomwa na Katibu wa Wizara ya Utalii Safina Kwekwe, alimwomboleza Bi Chidzuga kama kiongozi mwenye bidii ambaye daima alipigania haki za wasichana na wa wanawake.

Wakati wa kifo chake, alikuwa akihudumu kama mkurugenzi wa Bodi ya Maeneo Maalum ya Uchumi.Akihutubia waombolezaji Bw Mungaro alisema kabla ya kifo chake, Bi Chidzuga alikuwa na mipango ya kuwania kiti cha ubunge eneo la Matuga.

You can share this post!

Benzema aongoza Real Madrid kuzamisha chombo cha Alaves...

Watu 20 waangamia katika mlipuko wa tangi la mafuta Lebanon