Michezo

Wanasoka 7 waliotemwa na Liverpool na wakaishia kuwa masupastaa kwingineko

November 12th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

LIVERPOOL waliibuka mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2019-20 kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

Katika kipindi hicho cha kusubiri ufalme wa taji la EPL, miamba hao wa soka walishuhudia idadi kubwa ya wanasoka wakija na kuondoka uwanjani Anfield.

Kati ya wachezaji walioruhusiwa na Liverpool kuagana nao waliishia kuwa masogora wa haiba kubwa kwingineko. Baadhi yao ni hawa:

CONOR COADY

Aliingia katika sajili rasmi ya Liverpool mnamo 2005 akiwa na umri wa miaka 12 pekee. Alijitahidi na kupata uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Liverpool ambao walimwajibisha mara mbili pekee katika EPL.

Baada ya kutumwa kambini mwa Sheffield United kwa mkopo mnamo 2013-14, Coady alitiwa mnadani na akasajiliwa na Huddersfield Town aliowachezea mara 45 kwenye Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship).

Alijiunga baadaye na Wolves na kuwasaidia kupanda ngazi hadi kwenye EPL na kushiriki pia soka ya bara Ulaya. Kuimarika kwa makali yake akiwa Wolves ni kiini cha kuteuliwa kwake kuunga kikosi cha kwanza cha Uingereza dhidi ya Denmark mnamo Septemba 2020.

Aliridhisha zaidi kwenye mchuano huo uliomshuhudia akitawazwa mchezaji bora kabla ya kuongoza Uingereza, ambao kwa sasa wamechezesha mara tatu, kupepeta Wales 3-0 kirafiki mwishoni mwa Septemba.

PETER GULACSI

Kipa huyu raia wa Hungary alihudumu kambini mwa Liverpool kwa miaka sita. Hata hivyo, hakuwajibishwa katika mechi yoyote, mara nyingi akipangwa kuwa kipa chaguo la pili au la tatu nyuma ya walinda-lango Pepe Reina na Brad Jones.

Gulacsi alitumwa baadaye kuchezea Hereford, Tranmere na Hull City kwa mkopo kabla ya kuuzwa kambini mwa RB Salzburg mnamo 2013.

Baada ya kufufua makali yake katika Ligi Kuu ya Austria, kipa huyo aliyoyomea Ujerumani kuvalia jezi za RB Leipzig inayoshiriki Ligi Kuu ya Bundesliga.

Gulacsi kwa sasa amewadakia Leipzig kwa misimu mitano akiwa kipa chaguo la kwanza na amewasaidia kuendeleza ushindani mkali katika Bundesliga na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Hapana shaka kwamba Liverpool wangetamani sana kuwa na kipa matata kufu ya Gulacsi kwa sasa ili atoe ushindani mkali zaidi kwa nyota wao Alisson Becker.

RAHEEM STERLING

Alisajiliwa na Liverpool mnamo 2010 baada ya kuvalia jezi za Queens Park Rangers (QPR) kwa miaka saba.

Aligonga vichwa vya habari mnamo 2011 alipofunga mabao matano na kuwaongoza Liverpool kuwapepeta chipukizi wa Southend 9-0.

Sterling alianza kuchezeshwa katika kikosi cha kwanza cha Liverpool mnamo 2012 na akawajibishwa kwa kipindi cha misimu mitatu pekee. Japo aliondoka Liverpool akiwa tayari anajivunia jina kubwa katika ulingo wa soka, hapana shaka kwamba Sterling ameboreka zaidi tangu atue ugani Etihad kuchezea Manchester City ya kocha Pep Guardiola.

Akiondoka Liverpool, Sterlinga hakuwa amenyanyua taji lolote. Lakini kwa sasa amewaongoza Man-City kutwaa mataji mawili ya EPL, Kombe la FA na mataji manne ya League Cup.

Kati ya mabao 13 ambayo Sterling amefungia Uingereza, 12 yamepachikwa wavunia akiwa mwanasoka wa Man-City.

ALVARO ARBELOA

Beki huyu raia wa Uhispania alihudumu Liverpool kwa misimu miwili pekee, akiwa kizibo cha Steven Finnan katika mingi ya michuano.

Mnamo 2008-09, Arbeloa aliimarika zaidi na akayoyomea Uhispania kuchezea Real Madrid waliompa hifadhi uwanjani Santiago Bernabeu kwa miaka saba. Katika kipindi hicho, alipangwa mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Uhispania.

Alichezea Real mara 233 na kuwaongoza kutia kapuni taji moja la La Liga na mawili ya UEFA. Alichezea Uhispania mara 56 na kuwasaidia kutwaa mataji mawili ya Euro (2008, 2012) na Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini.

IAGO ASPAS

Aspas alichezea Liverpool mara 14 bila kufunga bao lolote. Atakumbukwa zaidi na mashabiki wa Liverpool kwa masihara yake ya 2013-14 dhidi ya Chelsea – mechi iliyochangia kushindwa kwao kutwaa taji la EPL.

Aspas aliagana na Liverpool baada ya msimu mmoja pekee na akatua Sevilla kabla ya kurejea Celta Vigo waliompokeza malezi ya soka katika umri mdogo.

Tangu wakati huo, amefunga mabao 92 katika La Liga kutokana na mechi 172 na kupokezwa fursa ya kuchezea timu ya taifa ya Uhispania mara 18. Alifunga bao muhimu katika sare ya 2-2 iliyosajiliwa na Uhispania dhidi ya Uingereza mnamo 2016. Aspas alikuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Uhispania kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mnamo 2018.

SUSO FERNANDEZ

Suso alijiunga na Liverpool mnamo 2010 baada ya kuagana na Cadiz. Hata hivyo, ilimchukua miaka miwili kabla ya kukwezwa ngazi hadi kikosi cha kwanza cha Liverpool.

Baada ya kuchezea waajiri wake mara 14 pekee kwenye msimu mmoja wa EPL, Suso alitumwa kuvalia jezi za Almeria kwa mkopo. Huduma zake zilinadiwa baadaye hadi AC Milan baada ya kuchezea Genoa mara tano pekee kwa mkopo. Hata hivyo, tangu 2016, Suso amekuwa supastaa huku akiwa tegemeo kubwa ugani San Siro kwa misimu mitatu na nusu kabla ya kutua Uhisapnia kuchezea Sevilla. Suso alikuwa sehemu ya kikosi cha Sevilla kilichozamisha Inter Milan kirahisi mwishoni mwa msimu wa 2019-20 na kutwaa ufalme wa Europa League.

DANNY INGS

Alijiunga na Liverpool mnamo 2015 akijivunia kuwa miongoni mwa wafungaji bora zaidi katika timu ya chipukizi nchini Uingereza.

Hata hivyo, Ings alichezea Liverpool mara 14 pekee katika mechi za EPL katika kipindi cha miaka minne ugani Anfield. Alikuwa mwepesi wa kupata mejaraha mabaya.

Alinunuliwa na Southampton mnamo 2019 waliojivunia huduma zake kwa mkopo wa mwaka mmoja ugani St Mary’s. Tangu apokezwe mkataba wa kudumu kambini mwa Southampton, Ings amefungia kikosi hicho mabao 26 kutokana na mechi 43 za EPL.

Mabao 22 aliyoyafunga katika msimu wa 2019-20 yalimkosesha kidogo (kwa goli moja pekee) fursa ya kutawazwa Mfungaji Bora wa EPL.

Ings kwa sasa amepata uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Uingereza, akifunga bao katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Wales na kuchangia magoli mengine mawili hadi kufikia sasa msimu huu.