Wanasoka chipukizi wafaidika kwa Sh16milioni baada ya kung’aa uwanjani

Wanasoka chipukizi wafaidika kwa Sh16milioni baada ya kung’aa uwanjani

NA JOHN ASHIHUNDU

Wanasoka chipukizi 120 wasiozidi umri wa miaka 20 wamechaguliwa kujiunga na kituo cha kunoa vipaji cha Barasa Foundation Soccer Academy.

Wachezaji hao walipatikana baada kung’ara wakati wa mashindano ya kuwania ubingwa wa Basara Foundation Champioship katika Kaunti ya Kakamega.

Mbali na kunufaika kutoka na maandalizi ya kituoni, kadhalika wachezaji hao wamepata ufadhili wa jumla ya Sh16 milioni kutoka kwa Chuo Kikuu cha Zetech University.

Mashindano hayo yaliyomalizika wikendi iliyopita yalivutia timu 1,234 kutoka maeneo yote 12 ya ubinge ambayo ni Shinyalu, Ikolomani, Khwisero, Navakholo, Likuyani, Lugari, Lurambi, Butere, Malava, Mumias East, Mumias West na Matungu.

Mshirikishi Mkuu wa mashindano hayo, Edward Omung’ala alisema wachezaji hao wataanza maandalizi mwezi April na kuendelea kujinoa wakati wa likizo za shule nchini, huku wakisubiri Makala mapya ya michuano hiyo kuanza mwezi Oktoba, mwaka huu.

Boniface Ambani mshambuliaji mstaafu wa aliongoza wenzake 10 waliovuma miaka ya hapo awali katika shughuli za kutambua vipaji bora wakati wa mechi hizo zilizofanyika kwa miezi mitatu, kuanzia mashinani.

Ambani alisema waliochaguliwa kujiunga na kituo hicho cha kunoa vipaji watafanyishwa mazoezi mbali mbali pamoja na kushiriki katika mechi za kujipima nguvu wakati wakifuatiliwa kwa makini na makocha wahusika.

Baada ya kukamilisha mafunzo hayo, Ambani alisema watasaidiwa kujiunga na timu za soka ya kulipwa hapa nchini na kule ng’ambo.

“Watapata fursa ya kucheza dhidi ya timu kubwa, mbali na kupokea mafunzo ya kiwango cha juu kutoka kwa klabu kubwa za ng’ambo.

Omung’ala alisema wanapanga kuandaa mashindano makubwa zaidi msimu ujao baada ya kuathiriwa na janga la Covid-19. “Tunataka idadi ya timu za kike ipande huku tukilenga kuwapa ufadhili wa kutosha wote watakaoshiriki. Kadhalika tutaandaa mafunzo ya kiufundi kufaidi makocha ambao hawajapata mafunzo yanayofaa.”

Barasa kupitia kwa mradi huo alisema ataendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha maisha ya vijana na akina mama katika kaunti nzima ya Kakamega yamebadilika. “Lengo letu ni kuimarisha kandanda kuanzia mashinani katika viwango tofauti.”

Wakati wa mechi hizo timu ya Asec FC ikiongozwa na Patrick Mugata iliilaza Ex-Internationals 1-0 katika pambano la maonyesho.

Barasa aliyeandamana na mkewe Janet alisema eneo la Magharibi limebarikiwa vipaji vingi vya hali ya juu huku akiwataja akina Victor Wanyama, Ayub Timbe na MacDonald Mariga kuwa miongoni mwa wachezaji walionufaika pakubwa kutokana na talanta zao.

Mbali na kusaidia vijana kupitia michezoni, Barasa Foundation iliyoanzishwa 2010 imekuwa ikiwasaidia vijana kwa kuwapa pikipiki ambapo kufikia sasa zaidi ya 500 wamepokea vifaa hivyo kote kwenye kaunti hiyo.

Timu ya Maroon FC kutoka Khwisero ndiyo iliyotwaa ubingwa huo kwa upande wa timu za kiume baada ya kuitandika Solofa FC ya Matungu 2-0 fainalini.

Ushindi huo uliwapa pesa taslimu Sh1.2 milioni. Solofa waliondoka na Sh600,000, huku Rangers FC kutoka Lurambi na All Stars ya Mumias Magharibi zikipewa Sh300,000 na Sh100,000 mtawaliwa kwa kumaliza katika nafasi za tatu nan ne mtawaliwa.

Taji la akina dada lilinyakuliwa na Lugari Progressive ya Mumias Mashariki ambao waliondoka na Sh500,000, Mwira FC kutoka Matungu wakipokea S250,000, Butali Starlets ya Malava Sh100,000 huku Wembe Starlets kutoka Lugari ikipata Sh50,000.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Aina mbalimbali za malipo na...

LISHE: Ugali na dagaa