Wanasoka wa Chelsea na Bayern Munich wabeba Ujerumani dhidi ya Iceland

Wanasoka wa Chelsea na Bayern Munich wabeba Ujerumani dhidi ya Iceland

Na MASHIRIKA

WANASOKA wawili wa Chelsea – Antonio Rudiger na Timo Werner – walifunga mabao mawili yaliyosaidia Ujerumani kuponda Iceland 4-0 katika mchuano wa Kundi J kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia za 2022.

Beki Rudiger alifunga bao lake kupitia mpira wa kichwa katika dakika ya 24 kabla ya Werner kushirikiana vilivyo na Kai Havertz ambaye pia ni mchezaji wa Chelsea na kupachika wavuni goli la nne la Ujerumani mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mabao mengine ya Ujerumani yalijazwa kimiani na wachezaji wawili wa Bayern Munich – Serge Gnabry na Leroy Sane katika dakika za nne na 56 mtawalia.

Ushindi huo uliwezesha Ujerumani waliotwaa Kombe la Dunia mnamo 2014, kudhibiti kilele cha Kundi J kwa alama 15, nne zaidi kuliko nambari mbili Armenia waliolazimishiwa na Liechtenstein sare ya 1-1.

Kwa mujibu wa wachanganuzi wa soka, mbinu za kocha mpya wa Ujerumani, Hansi Flick, zimekumbatiwa vilivyo na wanasoka wake ambao wanahusiana naye kwa karibu mno tofauti na hali ilivyokuwa wakati wa mkufunzi Joachim Loew aliyejiuzulu mnamo Julai baada ya fainali za Euro 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KAMAU: Vyombo vya habari vyafaa viwajibike 2022 ikikaribia

AKILIMALI: Punda ni ofisi yake; anawauza kwa wanaosaka...