Michezo

Wanasoka wa Harambee Stars kuanza mazoezi Kasarani

October 3rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WACHEZAJI wa Harambee Stars wanaopiga soka katika vikosi vya humu nchini wanatarajiwa kuingia kambini hapo kesho kwa minajili ya mchuano wa kirafiki utakaokutanisha Kenya na Zambia uwanjani Moi, Kasarani mnamo Oktoba 10.

Kocha Francis Kimanzi alitaja kikosi cha wanasoka 34 mwanzoni mwa wiki hii kwa minajili ya mechi nne zijazo za Stars, zikiwemo mbili dhidi ya Comoros katika safari ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Stars watavaana na Comoros katika mkondo wa kwanza jijini Nairobi mnamo Novemba 9 kabla ya kurudiana na kikosi hicho jijini Moroni siku nne baadaye.

Kabla ya kupigwa kwa mechi hizo za mikondo miwili dhidi ya Comoros katika Kundi G linalojumuisha pia Togo na Misri, Stars watakuwa wamepimana nguvu na Zambia na Sudan.

Wanasoka watakaotegemewa na kocha Francis Kimanzi katika mechi hizo, watakuwa wakiishi katika Safari Park Hotel, Nairobi.

“Kikosi kitapiga kambi ugani MISC Kasarani kuanzia Jumapili ya Oktoba 4. Wizara ya Michezo na ile ya Afya zimeishinisha mchakato huu wa kukutanisha wachezaji licha ya kanuni zilizopo za kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Barry Otieno.

Hofu ya pekee kwa kocha Kimanzi ni kwamba wanasoka wote wa humu nchini atakaokuwa nao kambini wamekuwa nje kwa kipindi kirefu tangu shughuli zote za soka ya humu nchini zisitishwe mnamo Machi 2020 kwa sababu ya Covid-19.

Kwa mujibu wa Otieno, FKF imepania kuhakikisha kwamba kanuni zote zilizopo za kudhibiti maambukizi ya corona zinatekelezwa ipasavyo na maafisa pamoja na wachezaji kambini na hata hotelini.

“Tunalenga pia kuandika barua kwa serikali kupitia Wizara ya Michezo ili itupe fedha za kufanikisha shughuli ya kuwafanyia maafisa na wanasoka walioitwa kambini vipimo vya corona kuanzia Jumatatu wiki ijayo,” akaongeza

Awali, kulikuwa na suitafahamu iwapo Stars wameshiriki mechi zijazo za kufuzu kwa fainali za AFCON dhidi ya Comoros baada ya serikali kutaja soka kuwa miongoni mwa michezo iliyohitaji wachezaji kugusana kinyume na masharti yaliyopo ya kudhibiti msambao wa corona.

Hata hivyo, Waziri wa Michezo, Amina Mohamed aliahidi kusaidia Stars kushiriki michuano hiyo muhimu.