Michezo

Wanasoka wa klabu za La Liga kuanza mazoezi ya pamoja katika makundi ya watu 10

May 17th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KLABU za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) zinatarajiwa kuanza mazoezi ya pamoja katika makundi mnamo Mei 18, 2020, katika jitihada za kujiandaa kwa marejeo ya kipute hicho mnamo Juni 12.

Wachezaji wote wa ligi hiyo walirejea kambini wiki mbili zilizopita na kila mmoja akawa anajifanyia mazoezi baada ya kupimwa ili kubaini iwapo wana virusi vya corona au la.

Ni wanasoka watano wa soka ya Uhispania waliopatikana na virusi hivyo hatari. Watano hao ambao majina yao yalibanwa, hawakuwa wakionyesha dalili zozote za kuugua corona kabla ya kufanyiwa vipimo hivyo vya afya.

Walitengwa na wamekuwa wakipimwa mara kwa mara huku wanathibitishwa kupona wakiruhusiwa kuungana na wenzao katika kambi husika za mazoezi.

Kwa mujibu wa Javier Tebas Medrano ambaye ni Rais wa La Liga, wachezaji wa vikosi vyote 20 wa ligi hiyo watashiriki mazoezi katika vikundi vya wanasoka wasiozidi 10.

Hatua itakayofuata itakuwa ni mazoezi ya pamoja kwa wanasoka wote wa kila kikosi kambini kabla ya mechi za zilizosalia muhula huu kutandazwa ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki.

Ingawa awali ni wachezaji wanane pekee ndio waliotakiwa kuunga kila kundi, idadi hiyo iliyoongezwa hadi kufikia 10 baada ya mashauriano kati ya vinara wa soka, serikali ya Uhispania na maafisa wa afya.

Uchache wa wachezaji na maafisa wa soka ambao wamepatikana na virusi vya corona hadi kufikia sasa katika ligi za Uhispania unamaanisha kwamba hapana ulazima wa kuwazuilia wote katika kambi zao.

Hivyo, wachezaji na maafisa hao wataruhusiwa kutokea nyumbani kwa ajili ya mechi na kurejea mwishoni mwa mapambano.

Uhispania ndilo la taifa la pili baada ya Italia katika bara Ulaya kuathiriwa zaidi na janga la corona baada ya maambukizi zaidi ya 225,000 kuripotiwa na zaidi ya vifo 27,000 kutokea kufikia Mei 17, 2020.