Michezo

Wanasoka watano wa ligi za nchini Uhispania waugua Covid-19

May 10th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WACHEZAJI watano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na Ligi ya Daraja ya Kwanza (Segunda) wamepatikana na virusi vya corona.

Watano hao ambao vinara wa soka ya Uhispania wamebana majina yao, hawakuonyesha dalili zozote za kuugua corona kabla ya kufanyiwa vipimo vya afya.

Kwa sasa wametengwa na watakuwa wakifanyiwa vipimo vya mara kwa mara hadi watakapothibitishwa kupona kisha waruhusiwe kuungana na wenzao katika kambi husika za mazoezi.

Viongozi wa La Liga walianza kuwapima wanasoka nchini Uhispania wiki jana, hii ikiwa sehemu ya mahitaji ya kimsingi yanayostahili kufanywa na klabu zote katika juhudi za kurejelewa kwa kampeni za soka msimu huu.

Kivumbi cha Ligi Kuu ya Uhispania kilichositishwa mwanzoni mwa Machi 2020 kutokana na janga la corona, kinatazamiwa kuanza upya mnamo Juni 12 na kutamatika mwanzoni mwa Julai 2020.

Kati ya klabu 20 za Ligi Kuu ya Uhispania, 13 ikiwemo Barcelona zilirejea kambini wiki iliyopita huku kila mchezaji akiruhusiwa kujifanyia mazoezi kivyake.

Uhispania ni miongoni ndilo la taifa la pili baada ya Italia katika bara Ulaya kuathiriwa zaidi na janga la corona baada ya maambukizi zaidi ya 224,300 kuripotiwa na zaidi ya vifo 26,600 kutokea kufikia Mei 10, 2020.

Kwingineko barani Ulaya, mchezaji wa tatu katika kikosi cha Brighton kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) alipatikana na virusi vya corona.

Klabu ya Dynamo Dresden inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Ujerumani (Bundesliga 2) imewaweka wachezaji wote na benchi nzima ya kiufundi katika karantini ya siku 14 baada ya masogora wawili kupatikana na virusi vya corona.

Serikali ya Ureno inatazamiwa pia kutoa mwongozo mpya kuhusu kurejelewa ka Ligi Kuu ya taifa hilo baada ya wanasoka watatu wa kikosi cha Vitoria Guimaraes kuugua corona.