Habari Mseto

Wanaume 2 wafa wakizozania Sh50

November 23rd, 2020 2 min read

Na OSCAR KAKAI

WANAUME wawili wenye umri wa makamo walipoteza maisha baada ya kupigania Sh50 katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Wawili hao walikuwa wamelipwa pesa hizo baada ya kushukisha mahindi kutoka kwa lori mjini Makutano.

Mmoja alimuua mwenzake walipopigana Jumapili jioni, ndipo umati uliokuwa na ghadhabu ukamvamia muuaji kwa kumpiga kwa mawe na fimbo hadi akajeruhiwa vibaya na kufariki.

Miili ya wawili hao iliachwa uwanjani ambapo wakazi walifurika kujionea, kabla ya maafisa wa polisi kufika na kutuliza hali baadaye.

Tukio hilo liliwaacha wakazi na mshutuko huku baadhi ya wakazi wakishangaa kwa nini watu ambao wamekomaa walishindwa kusuluhisha tofauti zao bila kusababisha maafa.

Kulingana na baadhi ya walioshuhudia mkasa huo, wawili hao walilipwa Sh50 lakini wakakosana kuhusu ni nani anafaa kupata hela nyingi kumliko mwenzake.

Bw Josiah Kodungura ambaye alishuhudia kisa hicho, alisema kuwa wawili hao walikuwa wamegombana wiki iliyopita walipofanya kazi hiyo ya kubeba mizigo na mauti yao yalisababishwa na hasira walizokuwa wamewekeana.

“Wiki iliyopita walikosana kuhusu fedha. Mmoja wao alikuwa akitembea na kisu akitishia kumuua mwenzake. Alikuwa na kisasi kuhusu fedha ambazo walikuwa wamelipwa baada ya kuweka na kushukisha mahindi kwenye lori wiki iliyopita,” alisema.

Aliongeza kusema kuwa wawili hao walianza kupigana lakini umati uliwapuuza hadi wakati mmoja wao alitoa kisu kutoka kwa mfuko wa long’i yake na kumdunga mwenzake kifuani kisha akaanguka kando ya barabara akivuja damu.

“Baada ya kumdunga, aliamua kukimbia lakini alikamtwa na umma akapigwa hadi akafa,” alisema.

Bi Mary Lokir alisema inashangaza kuwa Sh50 zinaweza kuchangia kifo.

“Hii ni tabia mbaya. Wamewaacha wake zao sasa nani atawalinda? Ni aibu Sh50 kuleta vifo kwa dakika chache,” alisema.

Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Pokot Magharibi, Bw Jackson Tumwet alithibitisha mauaji hayo akisema kuwa bado watu hao hawajatambuliwa na familia zao.

“Mkasa huo ulitendeka majira ya jioni. Wawili hao walipigana suala ambalo lilisababisha mauti yao. Maafisa wa polsi walipokea habari kuwa kuna mtu ambaye alidungwa na kisu akaaga dunia walikimbia kwenye eneo la mkasa,” alisema Bw Tumwet.

Alisema kuwa washukiwa walipelekwa na polisi hospitali ya kaunti ya Kapenguria ambapo ilithibitishwa wamefariki.

Alisema kuwa miili yote ilipelekwa kwenye hifadhi ya maiti katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria ikingojea kufanyiwa upasuaji ili kutambua chanzo cha vifo huku maafisa wa polisi wakiendelea na uchunguzi.

Aliwashauri vijana kukoma kujihusisha na vita ambavyo vinaleta vifo.