Habari Mseto

Wanaume 4 kizimbani kwa kumteka nyara polisi wa kike

November 16th, 2018 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

WATU wanne wamekamatwa na kufikishwa kortini kwa tuhuma za kujaribu kumteka nyara na kumdhulumu polisi wa trafiki wa kike.

Benson Omusula, Robinson Wamusolo, Phanice Nasimiyu na Sharon Naliaka wanadaiwa kumteka nyara Koplo Ann Rono karibu na daraja la Mto Nzoia katika barabara ya Mumias kuelekea Bungoma wakiwa na nia ya kumuua.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Novemba 13,2018.

Mahakama iliambiwa afisa huyo alijeruhiwa shingoni na kifuani aliposhambuliwa na wanaume hao.

Afisa huyo alikuwa pamoja na wenzake ambao kwa pamoja walikuwa wanakagua magari katika kizuizi cha barabara katika kituo cha kibiashara cha Lukoye. Walikamata gari moja aina ya Nissan ambalo walishuku lilikiuka sheria za barabara kama sehemu ya operesheni ya kupambana na magari mabovu ya uchukuzi wa abiria.

Gari hilo ambalo kio chake cha mbele kilikuwa kimepasuka kidogo liliburutwa hadi katika kituo cha polisi cha Mumias ili dereva wake akichukuliwe hatua kwa kuvunja sheria za trafiki.

Lakini ghafla dereva na abiria walipokonya polisi huyo (Bi Rono) simu yake na wakatoroka ndipo mwathiriwa na wenzake wakawafuata unyo unyo.

Maafisa wengine na wahudumu wa boda boda walifuata gari hilo na wakafaulu kulikamata.