Habari Mseto

Wanaume 5 kinyang'anyironi kujaza nafasi ya Njiraini KRA  

May 28th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) imeorodhesha majina ya watu watano watakaochukua mahala pa John Njiraini ambaye muda wake wa kuhudumu kama kamishna mkuu umeisha.

Wote walioorodheshwa na mamlaka hiyo Jumanne ni wanaume. Julius Waita Mwatu, Richard Boro Ndung’u, Andrew Kazora Okello, James Githii Mburu na Duncan Otieno Onduru watajitosa kwa kinyang’anyiro cha kujaza nafasi hiyo.

Kulingana na KRA, kufikia mwishoni mwa muda wa kutuma maombi, watu 30 waliomba ambapo wanawake walikuwa wawili pekee.

“Maombi hayo yalichunguzwa kuhakikisha kuwa yametimiza mahitaji. Bodi ya KRA ilipitisha majina ya waombaji watano watakaofanya mahojiano ya mwisho,” ilisema KRA katika tangazo.

Mamlaka hiyo inawataka wote walio na habari kuhusiana na walioorodheshwa kuiwasilisha ili kuisaidia kuchagua kamishna mkuu bora zaidi kabla ya Mei 31.

Bw Njiraini alifikisha umri wa kustaafu kwa lazima wa miaka 60 Desemba 19, 2017 ila badala ya kuondoka, kipindi chake cha kuhudumu kilirefushwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Hii ni baada ya serikali kuondoa umri wa mwisho wa kustaafu kwa wasimamizi wa taasisi za serikali, baada ya Okiya Omtatah kufika mahakamani kusukuma kuondoka kwake.

Omtatah alijaribu kwa mara ya pili lakini hakufaulu. Kampuni ya Pricewaterhouse Coopers (PwC) ndiyo inayohusika katika kujaza nafasi hiyo.

Kuondoka kwa Njiraini na shughuli za kutafuta msimamizi mpya kulivutia sarakasi ambazo zilimfanya Rais Uhuru Kenyatta kuchukua hatua na kuwafuta wanachama wa bodi karibu wote.