WANAUME KAMILI

WANAUME KAMILI

Na LEONARD ONYANGO

WALIOKUWA majaji wakuu Willy Mutunga na David Maraga, wamejitokeza kuwa miongoni mwa Wakenya wachache walio na ujasiri wa kumwambia ukweli Rais Uhuru Kenyatta anapokiuka Katiba.

Hapo jana, Jaji Maraga aliwataka wabunge kuanzisha mchakato wa kumtimua Rais Kenyatta madarakani kwa kukaidi Katiba, siku moja tu baada ya Dkt Mutunga kumkashifu rais kwa kuhujumu utawala wa kisheria.

Jaji Maraga alitaja hatua ya Rais Kenyatta kukataa kuwateua majaji sita kama ukaidi wa hali ya juu wa Katiba, ambao adhabu yake ni kutimuliwa ofisini.

“Huo ni ukaidi mkubwa wa Katiba. Sasa ni jukumu la Bunge kutumia Kifungu cha 142 cha Katiba na kuanza mchakato wa kumng’oa ofisini. Hiyo ndiyo njia ya pekee ya kurejesha utawala wa sheria.

“Tukikubali Rais aendelee anavyoendelea kutakuwa na shida kubwa nchini kwa sababu hii itampa nguvu za kufanya mambo anavyotaka bila kuheshimu sheria. Katika demokrasia, hakuna mtu anaruhusiwa kufanya anavyotaka bila kuzingatia sheria,” akasema.

Jaji Maraga alisema hayo siku moja baada ya mtangulizi wake Willy Mutunga kumwandikia barua Rais Kenyatta akimshutumu vikali kwa kutumia vibaya mamlaka yake.

Kwenye barua yake, Jaji Mutunga alisema ni jambo la kutia wasiwasi wakati mazoea ya kukiuka Katiba yanapoingia katika taifa, hasa kutoka kwa rais.

“Ofisi ya serikali sio mali ya kibinafsi kwa mtu kufanya kila anachotaka… Katiba imeweka wazi utaratibu wa yeyote anayehisi kuwa hawezi kuheshimu Katiba kustaafu ama kujiuzulu ili kuilinda dhidi ya hujuma,” akasema Jaji Mutunga kwenye barua yake.

Akihojiwa na runiunga ya KTN jana, Jaji Maraga alisema kila afisa wa serikali anayekula kiapo cha kulinda Katiba anahitajika kufanya hivyo bila masharti.

RAILA AKOSOE UHURU

Pia alimtaka kinara wa ODM, Raila Odinga kumkemea Rais Kenyatta kwa kukiuka Katiba.

“Waliofanya mwafaka wa handisheki na rais wanastahili kuwa wa kwanza kumkosoa kwa kukiuka Katiba. Wanafaa kumweleza kwamba amekosea na anafaa kusikiza wanachosema Wakenya,” akasema Jaji Maraga.

Mnamo Juni 3, Rais Kenyatta aliteua majaji 34 kati ya 40 waliokuwa wamependekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) mnamo 2019.

Waliokataliwa na Rais Kenyatta ni pamoja na majaji wawili wa Mahakama Kuu waliokuwa kwenye jopo lilimzimia reggae ya BBI mwezi jana, ambao ni Joel Ngugi na George Odunga.

Wawili hao walikataliwa kuingia Mahakama ya Rufaa pamoja na Aggrey Muchelule na Weldon Korir.

Wengine ni Evans Kiago na Judith Omange ambao walifaa kuhudumu katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi.

Rais Kenyatta alisema kuwa alikataa kuwateua majaji hao baada ya kupokea “taarifa za kijasusi kuhusu uadilifu wao”.

Lakini jana, Jaji Maraga alipuuzilia mbali madai hayo, akisema kuwa Idara ya Ujasusi (NIS) haina mamlaka ya kuteua majaji.

Alimtaka Rais Kenyatta kuwateua majaji hao sita, kisha awasilishe ushahidi aliopata kutoka kwa NIS mbele ya JSC ili wang’olewe kutoka afisini kwa mujibu wa sheria.

Jaji Maraga alisema kuwa uamuzi huo wa Rais Kenyatta umewaharibia sifa majaji hao sita: “Wakenya sasa wanawachukulia majaji hao kuwa walio na dosari kimaadili na maamuzi wanayofanya yanatiliwa shaka.”

Alifichua kuwa kulikuwa na juhudi za Rais Kenyatta kuwazima baadhi ya majaji mnamo 2019 shughuli ya kufanya mahojiano ilipokuwa ikiendelea.

“Tulipokea taarifa kutoka Ikulu kwamba baadhi ya watu tuliokuwa tunawahoji walikuwa na dosari. Tuliwambia watuletee ushahidi ili tuwape wahusika fursa ya kujitetea kwa mujibu wa Katiba. Lakini afisi ya rais ilikataa kutuletea ushahidi iliodai kuwa nao.

“Bila ushahidi ilibidi tupuuze madai hayo ya Ikulu, kwani hayakuwa na mashiko na tukapendekeza majaji hao wateuliwe na rais,” Jaji Maraga akaambia runinga ya KTN kwenye mahojiano jana.

Alieleza kuwa baada ya kuwasilisha orodha ya majaji waliopendekezwa kwa rais, Ikulu ilirudisha baadhi ya majina kwa JSC ikidai kuwa baadhi yao hawakufaa, lakini kamwe haikuambatanisha ushahidi wa madai hayo.

“Lakini jambo la kushangaza ni kwamba baadhi ya majaji ambao walidaiwa kuwa na dosari waliteuliwa na rais wiki iliyopita, na wengine waliodaiwa kuwa safi wamekataliwa,” akasema Jaji Maraga.

Alimtetea mrithi wake, Martha Koome kwa kuhudhuria hafla ya kuwaapisha majaji 34 wiki iliyopita katika Ikulu ya Nairobi.

Alisema wakati wa uongozi wake alikataa pendekezo la kutaka kuteuliwa kwa majaji wachache.

 

You can share this post!

Beki Okumu avutia klabu bingwa barani Ulaya

Kocha Maurizio Sarri sasa kudhibiti mikoba ya Lazio kwa...