Wanaume makahaba waongezeka Mombasa

Wanaume makahaba waongezeka Mombasa

Na WINNIE ATIENO

TAHARUKI imetanda Kaunti ya Mombasa baada ya vijana kati ya umri wa miaka 19 na 23 kujitokeza na kutangaza hadharani namna wanavyosajiliwa na wanawake matajiri kula uroda nao katika hoteli za kifahari na majumba ya ukwasi eneo la Nyali.

Idadi ya wavulana wadogo wanaowekwa kimada na wanawake wenye umri wa makamo au hata zaidi inaongezeka katika mji wa kitalii wa Mombasa, suala linaloendelea kuzua taharuki eneo hilo.

Hata hivyo, baadhi ya vijana hao waliambia Taifa Leo kuwa walisukumwa kwenye biashara ya ngono kutokana na ugumu wa maisha wakati shughuli za kawaida zilipoyumbishwa na janga la corona.

“Nilijitosa katika tabia ya ukahaba sababu ya ukosefu wa ajira. Wale wanawake wana pesa, anakutumia teksi uende mahali aliko ama mnakutana hotelini. Ni biashara iliyo na pesa,” akasema kijana wa umri wa miaka 22 anayekiri kujiingiza kwa hiyo tabia.

Mtaani Bamburi, Shawn alisema alisajiliwa kwenye biashara hiyo na rafiki yake kwenye kikundi cha makahaba wanaume.

“Rafiki yangu alinijuza kuhusu biashara hii ya ngono na nikalipishwa Sh500 kuwa mwanachama wake. Msajili wetu hututafutia wateja. Kila mteja ninayepata huwa nalipwa Sh4,000 ikiwa chache lakini kazi ikiwa nzuri huwa nalipwa Sh7,000 kwa kila mteja,” afichua Shawn kutoka Bamburi.

Wapo wanaohisi biashara hii inayokiuka maadili imenasua vijana kutokana na uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, wapo waliojinasua kutoka mtego huo na kuanza kurekebisha tabia ya walionaswa na biashara hiyo.

“Wakati corona ilipoanza ndipo mambo yalipokuwa mabaya kwa sababu wazazi walikuwa wanang’ang’ana sana. Mzazi wangu alikuwa anafanya kwa hoteli lakini zilipofungwa akakosa ajira. Ikabidi aanze kwenda kuwaoshea watu nguo ili tupate riziki. Ikabidi nisake pesa ili nimsaidie mamangu,” alisema Jackson.

Wale waliohojiwa na Taifa Leo walisema kuna kundi la WhatsApp lenye vijana zaidi ya kumi, ambao wanashirikiana pamoja na mkubwa wao mwenye kuwahadaa na kuwaingiza kwenye biashara hiyo.

“Hpao ndipo wanatafutiwa wateja kupitia mitandao ya ngono au kuunganishiwa na jamaa huyo anayesemekana ni kiongozi wao. Hao wanawake huishi sehemu kama Nyali wanasema mabwana zao hawawezi shughli,” aliongeza kijana mwingine ambaye aliomba jina lake libanwe.

Baadhi ya vijana hao wamejinasua na kundi hilo na sasa ni wasanii wanaotoa nasaha kwa wenzao kuvuka sakafu

“Yaliyopita si ndwele tugange yajayo..mtu akinihukumu sababu ya maisha yangu ya hapo awali ni sawa. Lakini nimebadilika na wazazi wangu wamenikubali,” alisema Wandera.

Maryline Laini, Mkurugenzi wa Ikoko Iju Africa alisema wazazi wengi hawajui maisha ya watoto wao.

“Wazazi wengi hawajui watoto wao ni makahaba. Ni dharihiri kuwa idadi ya wanaume makabaha imeongezeka. Vijana wanasajiliwa kuingia kwenye biashara za ngono kati ya wanaume ambayo imekithiri katika fuo zetu,” akaeleza Laini.

Hata hivyo, vijana hao kwa sasa wanaendelea kupata ushauri na nasaha kutoka kwa shirika la Ikoko Iju Africa, ambalo lina lengo la kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwatoa kwenye maisha hayo.

You can share this post!

Onyo magaidi wasajili watoto mitandaoni

Mjane wa Waititu apewa tiketi ya Jubilee Juja