Michezo

Wanaume na wanawake wa Kenya waadhibiwa na Zimbabwe mashindano ya magongo kuingia Olimpiki

August 15th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NI rasmi sasa kuwa timu ya magongo ya wanaume ya Kenya imebanduliwa nje ya kampeni ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 2020 baada ya kulimwa 3-2 na Zimbabwe katika mechi yake ya tatu ya mchujo wa Afrika unaoendelea nchini Afrika Kusini.

Vijana wa kocha Meshack Senge waliingia mchuano huu wakiuguza vichapo dhidi ya Ghana (3-2) na Misri (7-2).

Jinsi ilivyofanya dhidi ya Ghana kupoteza uongozi mara mbili ikipigwa, ndivyo mambo yalikuwa tena Kenya iliposhuka uwanjani kumenyana na Zimbabwe, Alhamisi.

Festus Onyango aliweka Kenya mbele 1-0 kutokana na kona fupi dakika ya 20. Mabao yalikuwa 1-1 katika robo ya tatu baada ya Zimbabwe kusawazisha kutokana na kona fupi iliyokamilisha kwa ustadi na Tatenda Kanyangarara dakika ya 36.

Arnold Marango alirejesha Kenya juu 2-1 dakika ya 43, lakini Zimbabwe ilisawazisha tena 2-2 kupitia kwa Tendayi Maredza dakika ya 50. Maredza alizamisha kabisa matumaini finyu ambayo Kenya ilikuwa nayo dakika ya 56.

Baada ya vichapo hivi vitatu, Kenya, ambayo ilishiriki Olimpiki mara ya mwisho mwaka 1988 nchini Korea Kusini, sasa iko katika hatari ya kuvuta mkia katika mashindano ya kuchagua mwakilishi wa Afrika kwenye Olimpiki nchini Japan mwaka 2020.

Kenya, ambayo inashikilia mkia bila alama, itakabiliana na Afrika Kusini mnamo Agosti 17 na kukamilisha ziara yake dhidi ya Nambia mnamo Agosti 18.

Kabla ya wanaume wa Kenya kushangazwa na Zimbabwe, warembo wa Kenya pia hawakuwa na lao dhidi ya Zimbabwe baada ya kuchabangwa 2-0 na kutia doa kubwa katika juhudi zao ya kushiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza kabisa.

Wazimbabwe Roxanne Viviers na Nicola Watson walitikisa nyavu za Kenya katika dakika ya 44 na 51, mtawalia. Warembo wa kocha Tom Olal waliingia mchuano huu baada ya kutoka 1-1 dhidi ya Ghana na kuchapa Namibia 1-0 katika mechi zake mbili za kwanza. Watarejea uwanjani kukamilisha ratiba dhidi ya Afrika Kusini mnamo Agosti 17.