Habari za Kaunti

Wanaume sita washtakiwa kuiba simu ya Sh1,500

June 11th, 2024 1 min read

NA TITUS OMINDE

WANAUME sita wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa genge linalohangaisha wakazi wa mji wa Eldoret wameshtakiwa kwa wizi wa kimabavu wa simu ya rununu ya Sh1,500 na bidhaa nyingine za kielektroniki.

Mahakama iliambiwa Jumanne kuwa Timona Keya,19, Valentine Shitemi,24, Dennis Kelly,19, James Kiprotich,21, Bernard Shikanga,21, na William Monje,18, mnamo usiku wa Juni 7, 2024, kwa pamoja wakiwa mjini Eldoret waliiba simu moja ya mkononi aina ya Itel yenye thamani ya Sh1,500 na pesa taslimu Sh4,000 mali ya Bw Henry Muyanzi.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa vitisho vya kumjeruhi mwathiriwa wao kabla ya kutekeleza wizi huo.

Wakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Eldoret Peter Areri, wote sita walikiri shtaka hilo.

Washtakiwa hao walidai kuwa walilazimika kuiba simu kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, wakinuia kuiuza ili kupata fedha za kununulia chakula baada ya njaa kwa siku kadhaa.

“Nilimwibia simu na fedha mlalamishi kutokana na njaa iliyonisakama, nikawa ninataka pesa za kununua chakula. Lakini naahidi kutorudia kitendo kama hicho,” mshtakiwa mmoja aliambia mahakama.

Kiongozi wa mashtaka aliambia mahakama kuwa washtakiwa hao walikuwa wahalifu wa mara ya kwanza lakini akasisitiza kutoa adhabu kali ili kuwaonya vijana wengine wenye tabia kama hiyo.

Wakili wa serikali aliambia mahakama kuwa kesi sawa na hiyo zimekuwa zikiongezeka katika mji wa Eldoret.

Mahakama iliamuru maafisa wa idara ya urekebishaji tabia kuwasilisha ripoti ya muda wa majaribio mahakamani katika muda wa wiki moja kabla ya washtakiwa kuhukumiwa.

“Mahakama itawahukumu washtakiwa baada ya kupokea ripoti kutoka idara ya urekebishaji tabia,” akaamuru Bw Areri.

Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki moja.