Bambika

Wanaume wa SDA si washerati, asema mhubiri na kuvutia rundo la maoni

February 19th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

WANAMITANDAO wamemkosoa Pasta Boaz Ouma wa kanisa la wasabato (Seventh-day Adventist Church) wakitaka aelezee alipofanya utafiti uliomuaminisha kutoa kauli kwamba wanaume wa SDA si wadanganyifu.

Kwenye video iliyopakiwa katika chaneli ya YouTube na Facebook, Pasta Ouma alieleza uzoefu wa kuwa na Mungu kuwa sababu kuu ya wanaume katika kanisa hilo kutokuwa waongo.

“Kwa nini wanaume wa dini ya SDA si waongo? Jambo la kwanza, wana uzoefu fulani na Mungu. Hawako pale kwa sababu wako tuu… Kutoka mwanzo hadi walipo ni kwa sababu ya Mungu mwenyewe. Uzoefu huo hauwezi kuwafanya wajishushe kiwango cha chini au kujiingiza kwa tabia fulani itakayofanya kupunguza utukufu wa Mungu,” alijibu Pasta Ouma.

“Uzoefu wa kuwa kwenye dini unafanya kukosa kudanganya. Inawafanya kuwa waaminifu na kujitolea kwenye kazi ya Mungu,” aliongeza Pasta Ouma.

Kwenye video hiyo, ujumbe huo uliwaacha washiriki waliokuwa wamehudhuria ibada vinywa wazi.

Chapisho hilo lilivutia hisia, wanamitandao wakihitaji ufafanuzi zaidi kuhusu neno udanganyifu au uongo.

“Alifanya uchunguzi huu lini,” aliuliza Sharon Chebet.

“Ni vyema kufanya utafiti kabla ya kuja mbele ya umma na ujumbe mzuri,” alisema Geoffrey Ruto.

Joy Popolo alihisi kuwa ni wanaume wanaoamini Mungu ndio hawahusiki kwenye masuala ya aina hiyo.

“Si SDA pekee bali mtu yeyote anayemuogopa Mungu ana mipaka,” alichangia Joy Popolo.

Abby Rutto alifika kwenye ukurasa huo kuhadithia jinsi anavyoteseka na penzi ambalo hakujua.

“Nilikubali mmoja na mimi ni mwanasabato, sasa hivi nalia,” alisema Abby Rutto.

Wanjiru Kamau alimkosoa pasta huyo akidai kuwa ni wanawake pekee wanaofahamu wanaume wanaochepuka.

“Atí SDA? Kutoka wapi? Ni wanawake tuu wanaofahamu wanaume wagani wasiochepuka. Na mwingine alikua anataka kukuja sabato kwangu leo,” alisimulia Wanjiru Kamau.

“Kwa hivyo, nyie wanaume wa sabato si waongo? Wacha niangalie jina la mwingine hapa, mwenyewe nimfikishe jehanamu,” alitania Wanjiru Kamau.

Kwa mara nyingine dini ya wanasabato imegonga vyombo vya habari kwa kuwa na wahubiri ambao hawaogopi kuweka jumbe zao wazi kwa washirika wao.

Kanisa hilo lina Mhubiri Elizabeth Mokoro ambaye aliwahi kuelezea kisa cha shemeji yake akimtaka kuondoka kwenye ndoa.

“Pasta kwa nini unaendela kuishi na kaka yangu wakati unapitia mambo mazito,” aliuliza Shemeji ya Eizabeth Mokoro.