Habari

Wanaume wako hatarini kuambukizwa corona kuliko wanawake – Utafiti

March 23rd, 2020 1 min read

NA MARY WANGARI

DATA iliyokusanywa kufikia sasa kuhusu virusi vipya vya corona inaonyesha kwamba wanaume wanakabiliwa na hatari zaidi ya kuambukizwa COVID-19 kushinda wanawake.

Hii ni kulingana na Nikolay Briko, mkuu wa Idara ya kwanza ya Tiba kuhusu Mkurupuko na Ushahidi katika Chuo Kikuu Moscow na afisa wa Wizara ya Afya Urusi mnamo Jumatatu, Machi 23.

“Tukitazama nani anayepata virusi vipya vya corona, wanaume huambukizwa mara nyingi zaidi kushinda wanawake. Karibu mara mbili zaidi,”

“Sababu ya hali hii haijulikani. Huenda hii ni aina maalum ya hali ya kinga ya mwili, sifa ya kinga ya jinsia ya kiume na kike,” alisema mtaalam huyo.

Alizungumza wakati wa upeperushaji moja kwa moja wa kongamano lililoandaliwa kwa “Mustakabali wa Urusi.”

Alisema hajui iwapo aina ya damu inaweza kuathiri uwezo wa mtu kupata ugonjwa huo, hata hivyo, “kuna baadhi ya sifa za jeni zinazodhibiti uwezo na jinsi maambukizi yanavyokua.”

Boiko alieleza kwamba kiwango cha hatari cha ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona ni takriban asilimia 4.3.

“Janga ni wakati mkurupuko unapofikia takriban mataifa yote ulimwenguni. Kufikia sasa kuna mataifa 171, watu 14,706 wamefariki na visa vingine takriban 340,000 za ugonjwa huo vimethibitishwa. Kiwango cha hatari hufika asilimia 4.3. Kwa jumla, hii ni juu zaidi kiasi kushinda kawaida kwa maambukizi haya,” alieleza.

Alifafanua kuwa idadi hii huenda isiwe kamili maadamu inawezekana kwamba si visa vyote vya maambukizi vimerekodiwa.

“Si kila mtu amejumuishwa [katika idadi yote ya visa vya virusi vya corona), kwa mfano, kuna dalili ndogo zisizoonekana. Kungekuwa na watu zaidi walioambukizwa na kiwango cha hatari kitakuwa tofauti,” alieleza.

Mkurupuko huo unaosababishwa na virusi vya COVID-19 (vilivyokuwa vikifahamika mbeleni kama 2019-nCoV) uliripotiwa Wuhan, Uchina, mji mkuubwa wa kibiashara wenye watu 12milioni, mwishoni mwa Disemba 2019.

Visa vya virusi vipya vya corona pia vimeripotiwa katika mataifa na maeneo zaidi ya 150 ikiwemo Urusi ambayo kufikia sasa imerekodi visa 438.