Habari Mseto

'Wanaume wanapuuza kuvalia maski'

July 16th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

IDADI kubwa ya watu wasiovalia maski nchini ni wanaume, amesema Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Bw Kagwe Alhamisi amesema uchunguzi umeonyesha wanawake ndio wanatilia maanani uvaliaji maski, wakilinganishwa na wanaume.

“Ukitembea mijini na maeneo mbalimbali nchini utazame, utaona wengi wasiovalia maski ni wanaume. Idadi kubwa ya wanawake humu nchini wanapotembea hawakosi kuvalia maski,” waziri akasema wakati akitoa takwimu za maambukizi ya Covid-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Akasisitiza: “Ninahimiza Wakenya watilie mkazo sheria na mikakati iliyotolewa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu.”

Takwimu za mataifa mbalimbali ulimwenguni, Kenya ikiwemo, zinaonyesha wanaume ndio waathiriwa wakuu.

Waziri ametangaza kwamba visa vimepanda hadi 11,673 baada ya wagonjwa 421 zaidi kuthibitishwa kuugua.

Akizungumza katika kaunti ya Nakuru, Kagwe amesema idadi hiyo imebainika kutoka kwa sampuli 3,895 zilizofanyiwa vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Kati ya wagonjwa hao, 409 ni Wakenya huku 21 wakiwa raia wa kigeni.

Wanaume wamekuwa 297, wanawake 124.

Aidha, mgonjwa wa umri mdogo amekuwa mwaka mmoja, ule mkubwa akiwa na umri wa miaka 83.

Waziri Kagwe pia ametangaza kwamba wagonjwa 512 waliokuwa wakipokea matibabu nyumbani na kutunzwa wamethibitishwa kupona kabisa, na wengine 58 kuruhusiwa kuondoka katika vituo mbalimbali vya afya nchini, jumla idadi ya waliopona ikifika 3,638.

Idadi ya waliongamizwa na Covid-19 imefika 217, baada ya watu wanane kufariki kutokana na ugonjwa huu katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Kaunti zilizoandikisha visa vya virusi vya corona zimefika 42.