Habari Mseto

Wanaume watahadharishwa kuhusu corona

July 30th, 2020 1 min read

Na VALENTINE OBARA

WAZIRI wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, ametahadharisha wanaume kuhusu virusi vya corona akisema athari zake za baadaye hazijulikani.

Huku akionekana kurejelea fununu kwamba kuna uwezekano wa ugonjwa huo kusababisha matatizo kwenye sehemu za siri za wanaume, alisema wanaume wana kila sababu ya kujilinda dhidi ya maambukizi.

“Tumekuwa tukisikia fununu kutoka China… Sitaki nionekane kama mtu anayeeneza uvumi lakini inafaa wanaume wajihadhari hasa wale ambao wangali vijana. Katika miaka ijayo, hatujui haya magonjwa yatakuwa na athari gani,” akasema.

Alikuwa akizungumza Nairobi alipotangaza kwamba maambukizi mapya 544 yalipatikana, na kufikisha idadi ya jumla hadi 19,125.

Wagonjwa 12 walifariki na hivyo basi kufikisha idadi hadi 311. Lakini wengine 113 walipona, na kufikisha idadi yao hadi 8,021.

Kufikia sasa, idadi ya wanaume wanaoambukizwa imezidi ya wanawake, ingawa Bw Kagwe alisema pia idadi ya wanawake imeanza kuongezeka.

“Natumai wanawake hawajaanza kuzembea katika kufuata kanuni za kujiepusha maambukizi,” akaeleza.

Athari za ugonjwa wa Covid-19 bado huendelea kugunduliwa kadri na jinsi tafiti kuhusu ugonjwa huo zinavyoendelezwa kimataifa.

Kufikia sasa, tafiti zimethibitisha athari za kudumu kwa baadhi ya wagonjwa wa Covid-19 ni kama vile kuharibu mapafu, kusababisha matatizo ya moyo na kiharusi.

Kando na hayo, serikali sasa imekiri kuna uwezekano wa maambukizi kuongezeka katika msimu huu wa baridi.

Bw Kagwe alieleza kuwa, kwa vile msimu wa baridi husababisha homa ya kawaida, inawezekana watu wengi wanakosa kinga mwilini dhidi ya magonjwa ndipo wanaambukizwa virusi vya corona.

“Katika msimu huu ni muhimu tuepuke kabisa kukongamana,” akasema.

Alikashifu wahudumu wa afya ambao alisema wanakiuka kanuni za kupambana na ugonjwa huo na hivyo kuwaweka wagonjwa na umma kwa jumla taabani.

“Wakati wa vita, nidhamu ya juu zaidi hutakikana kwa wanajeshi walio katika mstari wa mbele. Nawaomba tafadhalini, tutende yale tunayosema,” akasema.