HabariSiasa

Wanaume watatu waliomhangaisha Moi

February 10th, 2020 3 min read

Na JOHN KAMAU

ALIYEKUWA Rais wa pili wa Kenya hayati Daniel Arap Moi alihangaishwa na kuaibishwa na maafisa watatu wa serikali waliokuwa wakihudumu Mkoa wa Rift Valley, yeye akiwa makamu wa rais wa Mzee Jomo Kenyatta.

Maafisa hao walikuwa Mkuu wa Mkoa Isaiah Mwai Mathenge, Mkuu wa Polisi James Erastus Mungai na Mhadisi wa Barabara Kim Gatende.

Mnamo usiku ambao Mzee Kenyatta alifariki, Bw Mungai aliripotiwa kuagiza vizuizi kuwekwa barabarani kati ya Nakuru na Nairobi kumzuia Moi kusafiri hadi Nairobi kuapishwa kuwa rais, lakini juhudi zake zikagonga mwamba.

Katika kisa kingine awali, Moi alikuwa ameitwa Ikulu ya Nakuru na Mzee Kenyatta, ambapo aliaibishwa na Bw Mathenge kwa kuachwa angoje kwa masaa mengi katika sehemu ya kupokea wageni, huku waliofika nyuma yake wakiruhusiwa kuingia kumwona rais.

Kulingana na Moi katika kitabu kilichoandikwa na Andrew Morton, Mzee Kenyatta alipopiga simu kuuliza kama kulikuwa na yeyote aliyebaki hajamuona, Mathenge alisema: “Ni Moi pekee yuko hapa.”

Mzee Kenyatta alienda eneo la kupokea wageni alikokuwa Moi na kuanza kuzungumza kwa Kikuyu, kisha akamwambia waingie ndani kusiza wanakwaya waliokuwa wakimtumbuiza ndipo baadaye wazungumze.

Mzee Kenyatta alishikwa na usingizi na kulala wakati wa utumbuizaji na hivyo Moi hakupata fursa ya mazungumzo na mkubwa wake.

Kulingana na Morton, Mungai alimzaba Moi makofi mara mbili mbele ya Kenyatta katika Ikulu ya Nakuru, ambapo inadaiwa alimlazimu pia kuvua nguo.

Moi alipolalamika kwa Kenyatta, Jomo alimuuliza nani alikuwa akisimamia polisi, ambapo wakati huo walikuwa chini ya Moi kama waziri wa masuala ya ndani.

Katika kisa kingine, siku moja Bw Mungai aliagiza polisi kusimamisha msafara wa Moi na kupekua magari yote.

Baadaye aliagiza ukaguzi nyumbani kwa Moi mjini Nakuru.

Mnamo 1975 Moi alikuwa amerudi nchini kutoka Kampala, Uganda wakati Bw Mungai alipodai alikuwa ameingiza silaha nchini akiwa na njama ya kupindua serikali ya Kenyatta.

Bw Mungai aliagiza polisi kutafuta silaha kwa kumkagua Moi mwenyewe na pia katika ofisi yake Nakuru.

“Moi alikuwa mwenye wasiwasi mkubwa. Kila jioni aliomba kwa hofu kuwa angeuawa wakati wowote,” anasema Morton kwenye kitabu kuhusu maisha ya Moi.

Bw Gatende naye akiwa mhadisi mkuu wa barabara Rift Valley, alihakikisha kuwa barabara ya kwenda nyumbani kwa Moi eneo la Kabarak imewekwa matuta mengi yasiyo na maana yoyote pamoja na vizuizi vingi kwa nia tu ya kumuaibisha Moi.

Bw Morton anasema kwenye kitabu chake kuwa baadhi ya rafiki zake Moi hawakuamini jinsi alivyoweza kuvumilia aibu na mateso aliyopitia mikononi mwa maafisa wa ngazi ya chini.

Wakati alipotwaa madaraka, Bw Mungai alitumwa kwenye likizo ya lazima na baadaye akatoroka Kenya akihofia Moi angelipiza kisasi kwa aliyomfanyia akiwa makamu wa rais.

Aliyekuwa Mkuu wa CID wakati huo Ignatius Nderi alisema Mungai aliuza gari lake aina ya Range Rover na kutorokea Juba, Sudan akiandamana na wanaume wawili kutoka Turkana. Kisha alichukua ndege na kutorokea Uswizi.

Akiwa Uswizi, Bw Mungai aliishi kwa hofu na wakati mmoja alituma barua kwa aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Geofrey Kareithi akimuomba amtetee kwa Moi na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo.

Kabla ya Bw Mungai kutoroka nchini, Bw Njonjo alikuwa amedai Bw Mungai alikuwa akiandaa kikosi ambacho kilipanga kuua Moi, Makamu wa Rais Mwai Kibaki na Njonjo mwenyewe.

NGOROKO

Bw Mungai alidaiwa kuwa na kikosi cha maafisa 250 wa kitengo cha kupambana na wezi wa mifugo kilichofahamika kama Ngoroko, madai ambayo alikanusha kwenye barua yake kwa Bw Kareithi.

Alijitetea kuwa kikosi hicho kilikuwa na nia njema na hakuwa na mpango ya kumdhuru yeyote mbali kukabiliana na majangili Rift Valley

Baada ya Moi kuchukua madaraka, Bw Mathenge aliwasaliti marafiki zake ndipo Moi akampa fursa ya kuendelea kuwa mkuu wa mkoa wa Rift Valley hadi 1980.

Mungai alirudi nchini baadaye na anaendeleza shughuli za kilimo Nakuru.

Baada ya kufutwa kazi Bw Mathenge alirudi kwao Nyeri ambako aliingia kwenye siasa na akachaguliwa mwenyekiti wa Kanu katika iliyokuwa wilaya ya Nyeri.

Mnamo 1988 Moi alikuwa amepanga kumwangusha Kibaki na alifanya hivyo kwa kuhakikisha mshirika wake Mathenge ameondolewa kwenye uongozi wa Kanu.

Bw Mathenge alikuwa amemkasirisha Moi kwa kuwaita “takataka” madiwani wa Nyeri waliokuwa wametoa mwito aondolewe kwenye uwenyekiti wa Kanu tawi hilo.

Mnamo Juni 1988 Moi alisafiri Nyeri na kuwataja Bw Mathenge na Bw Gatenda kama “watetezi wa wakoloni” waliorudi Nyeri kugawanya wananchi.

Moi alipokuwa akihutubu Bw Mathenge alikataa kusimama jina lake lilipotajwa kama ilivyokuwa kawaida wakati huo na baadaye yeye na Bw Gatende walifukuzwa Kanu.

Bw Gatende, ambaye alikuwa mzaliwa wa Murang’a alihamia Nyeri baada ya yeye na Bw Mathenge kufutwa kazi ambapo waliendeleza shughuli za kilimo hadi walipokufa mnamo 2006 wakiachana kwa wiki moja pekee.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, mateso na aibu aliyopata Moi kutoka kwa Mathenge, Mungai na Gatende ndiyo yaliyompa ujasiri wa kukabili changamoto alipochukua urais.