Habari za Kaunti

Wanaume watazama taarifa mjini wanawake wakienjoi ‘Soap Opera’ majumbani

February 28th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

KILA jioni utapata wanaume wakikongamana katika eneo la umma la Mkunguni kutazama taarifa za habari kupitia skrini kubwa iliyotundikwa hapo.

Hatua hiyo imeleta afueni kubwa majumbani kwani akina baba hawapiganii tena rimoti na mabibi au watoto wao wanaopendelea kutazama vipindi vya ‘Soap Opera’ kwenye televisheni.

Hata hivyo jana Jumanne hali ilikuwa tofauti kidogo katika mji huo ambao ni kitovu cha mji wa kale wa Lamu, kwani kulitokea hitilafu, wengi wakalazimika kutazama taarifa katika simu badala ya runinga.

Baadhi ya wanaume wakiwa wamekusanyika kutazama taarifa kwa simu ya mmoja wao baada ya kukosa televisheni ya Mkunguni mnamo usiku wa Februari 27, 2024. PICHA | KALUME KAZUNGU

Mkunguni ni eneo la umma lipatikanalo katikati ya mji wa kale wa Lamu. Eneo hilo lililoko chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Makavazi na Turathi za Kitaifa nchini (NMK) tangu jadi lilitengwa na kuwa la mikutano ya umma kutokana na jinsi lilivyo kitovu cha mji huo wa kihistoria.

Jina Mkunguni lilitokana na kuwepo kwa mti mkubwa wa Mkungu.

Kulingana na maelezo ya kimsingi ya kamusi, Mkungu ni mti unaozaa kungu ambazo ndani ya kokwa zake mna badamu.

Mti huo wa mkungu ulioko Mkunguni kisiwani Lamu unaaminika kudumu eneo hilo kwa zaidi ya miaka 100.

Mbali na jukumu hilo la kuandaa mikutano, iwe ya kisiasa, kitamaduni na mingineyo, siku za hivi karibuni Mkunguni imepokea umaarufu mwingine.

Hili ndilo eneo ambapo kila jioni utapata umma, hasa wanaume wakikongamana kutazama taarifa za habari, hasa zile za saa moja, kupitia skrini kubwa iliyotundikwa hapo.

Hatua hiyo imeleta afueni kubwa majumbani kwani akina baba hawapiganii tena rimoti na mabibi au watoto wao wanaopendelea kutazama vipindi vya ‘Soap Opera’ kwenye televisheni.

Unapopita eneo hilo la Mkunguni majira ya saa moja jioni, mara nyingi utapata wanaume wa kila tabaka, iwe ni matajiri au maskini, vijana kwa wazee, marafiki kwa maadui wakiwa wamekaa kitako wakifuatilia kwa karibu matukio ya siku kwenye skrini hiyo kubwa.

Bw Muhashiam Famau, mmoja wa wapenzi watazamaji wa taarifa za habari runingani, anasema hatua ya kuwekwa kwa skrini hiyo ya kuuwezesha umma kutazama televisheni bure bilashi Mkunguni ni yenye natija tele kwa jamii nzima.

Kulingana na Bw Famau, mbali na kupunguza mafarakano ndani ya nyumba, hasa kati ya bibi, watoto na bwana kuhusiana na kipi wangependa kukitazama runingani kwa wakati mmoja, kuwekwa kwa skrini ya Mkunguni pia kumesaidia familia zisizo na uwezo wa kumiliki televisheni pia kupata taarifa za habari na vipindi vingine punde wanapofika Mkunguni.

Bw Famau anashikilia kuwa kabla ya ujio wa mfumo wa skrini ya Mkunguni, mara nyingi wanaume majumbani wamejipata njia panda, hasa wakati wanapojibanza sebuleni kutaka kutazama habari kwenye televisheni zao.

“Unapata wewe kama mzee wa nyumba umekaa sebuleni kutaka kufahamu kilichojiri nchini na ulimwengu na kisha ghafla binvuu mtoto au mama anatokea na kubadilisha chaneli katika king’amuzi kile kufuatilia ‘Soap Opera’ zao. Twashukuru ujio wa skrini ya bure Mkunguni miaka ya sasa kwani umepunguza presha hizi za majumbani. Sisi wanaume sasa tumezoea kuishia kumiminika Mkunguni kutazama habari tukiachia mabibi na watoto televisheni nyumbani kutazama filamu zao. Hamna msongo tena,” akasema Bw Famau.

Bi Amina Bakari aliwashukuru walioibuka na mbinu ya kuonyesha habari za televisheni Mkunguni kila jioni, akisema hilo limechangia akina mama na watoto kuwa na uhuru wa ni kipindi kipi wangependa kutazama na kwa wakati gani.

Aliwahimiza waliokuja na mpangilio huo kutokoma kuonyesha taarifa Mkunguni, akishikilia kuwa waume wao huwa hawapendi mambo mengi kwenye televisheni ila tu hizo habari.

“Wanaume wetu wao sana hutaka habari ilhali sisi wake na watoto vyetu sana sana ni vipindi. Katu hatuwezi kuacha programu kama Sanura, Kina, Salem na nyinginezo kutupita tu hivyo eti kwa sababu kuna mtu anatazama habari kwenye hiyo televisheni yetu ya nyumbani. Hata waume wetu wanafahamu hilo. Utawapata ikikaribia au kugonga tu saa moja hivi wao wanachomoka kuelekea Mkunguni kutazama habari zao. Hilo ni afueni kubwa kwetu,” akasema Bi Bakari.

Mwanamke apita karibu na ubao wa kutandaza taarifa za runinga. Ubao huo mweupe ulitundikwa kwa ukuta wa jengo moja mjini Mkunguni. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Abdi Sharif, mpenzi mwingine mtazamaji wa habari za televisheni eneo la Mkunguni, aliwasifu waliokuja na wazo hilo la kuweka skrini ya kutazama taarifa kwa pamoja Lamu.

Bw Sharif anasema hata mara nyingine wakapewa uhuru wa kutazama habari hizo majumbani mwao, wengi hupendelea kumiminika Mkunguni kutazama taarifa kwa pamoja na wenzao huku wakibadilishana maoni kuhusiana na yale wanayojulishwa kwenye televisheni.

“Wengi wa wapenzi wa kutazama televisheni eneo la Mkunguni eti si kwa sababu tumenyimwa nafasi ya kufanya hivyo majumbani mwetu. Sisi hupendelea kuja Mkunguni kutangamana na marafiki. Tunatazama taarifa huku tukijadiliana masuala mawili au matatu muhimu ya kijamii na maendeleo ya nchi. Badala ya kujibanza sebuleni mwako kutazama taarifa ukiwa upweke, utamu ni kuja hapa Mkunguni kuzitazama hizo habari kwa pamoja tukiwa kundi zima bila kuboeka,” akasema Bw Sharif.

Hata hivyo jana Jumanne hali ilikuwa tofauti kidogo katika eneo hilo la Mkunguni, ambalo ni kitovu cha mji wa kale wa Lamu, kwani kulitokea hitilafu, wengi wakalazimika kutazama taarifa katika simu badala ya runinga.

“Tumefika hapa saa moja kamili kama kawaida kutazama taarifa ila tukavunjika moyo baada ya wasimamizi kukosa kuonyesha habari kwenye skrini kama ilivyo ada. Tumejulishwa kwamba kuna hitilafu kidogo ya kimitambo leo lakini wanarekebisha ili kesho tuendeleze ada yetu. Ndio manake unatuona tumejikusanya hapa kutazama habari kupitia simu tukijua fika kwamba kesho mambo yatakuwa sawa,” akasema Bw Sanita Safari.