Habari Mseto

Wanaume wawili wakamatwa Mombasa kwa kujifanya maafisa wa polisi

May 6th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

WANAUME wawili wanazuiwa katika kituo cha polisi cha Chaani eneobunge la Changamwe, Kaunti ya Mombasa kwa kosa la kujifanya maafisa wa polisi.

Wawili hao Stephen Obonyo na Mathew Onduru walikamatwa Jumanne, wakiwa wanawahangaisha wakazi eneo la Mlolongo.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi eneo la Changamwe Ali Ndiema amesema maafisa wa polisi walifaulu kuwakamata wawili hao baada ya kudokezwa na wakazi.

“Tulipokea habari kutoka kwa wakazi kuwa kumetokea kundi la watu ambao wanavalia makoti yaliyoandikwa ‘Shofco’ ambao wanasema kuwa ni maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Mikindani,” akasema kamanda huyo.

 

Stephen Obonyo (kushoto) na mwenzake Mathew Onduru wakiwa katika kituo cha polisi cha Chaani ambako wanazuiliwa. Picha/ Mishi Gongo

Amesema alituma maafisa wake mwendo wa saa kumi na mbili jioni ambao waliwatia mbaroni watu hao wakiwa katika shughuli ya kuhangaisha watu.

Aidha alisema watu hao wanatembea na mipira ambayo walitumia kuwachapa wakazi.

Amesema kwa sasa washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Chaani wakisubiri kufikishwa mahakamani Alhamisi.

Bw Ndiema amesema wawili hao watashtakiwa kwa kosa la kujifanya maafisa wa polisi na kujitayarisha kutekeleza uhalifu.