Makala

Wanaume wawili walivyofariki wakitoa ndoo kisimani kwa ahadi ya Sh200

June 1st, 2024 3 min read

NA OSCAR KAKAI

HAMU ya kutaka kupokea Sh200 iliishia majonzi wanaume wawili walipotumbukia kwa kisima katika boma moja mjini Makutano, kaunti ya Pokot Magharibi walipokuwa wakijaribu kutoa ndoo na kamba.

Wawili hao walikumbana na mauti ndani ya kisima cha kina cha zaidi ya futi 50 kwenye boma hilo lililo katika eneo la Lityei, mjini Makutano mnamo Jumanne.

Kufikia Jumatano, miili hiyo ilisalia ndani ya kisima huku juhudi za uokoaji zikiendelea. Mkuu wa Kituo cha polisi cha Kapenguria Lukas Wamocha, ambaye alithibitisha tukio hilo, alisema kuwa ilibidi waitishe maafisa wa kukabiliana na majanga kutoka jijini Nairobi kuondoa miili hiyo.

Mwathiriwa wa kwanza alitambulika kama Jonny, ambaye wenyeji walisema ni raia wa Uganda mwenye umri wa miaka 40, na ambaye ni mchimbaji visima katika eneo hilo aliyekuwa ameingia kwa kisima akilenga Sh200 kwa kazi ya kutoa ndoo na kamba.

Naye mwanamume wa pili alitambulika kuwa ni Joseph Rotich, 27, aliyetaka kulipwa Sh5,000 ili kuondoa mwili wa mtu wa kwanza.
Mikasa hii miwili ilitokea majira ya saa sita mchana katika boma la Bw Charles Kariuki.

Ilidaiwa kuwa wawili hao walikuwa waraibu wa pombe na kwamba walikufa kutokana na kukosa hewa ndani ya kisima.

Kulingana na Bi Helen Cheptum ambaye ni mkewe Bw Kariuki, kamba na ndoo vilianguka kwenye kisima chake Jumatatu na kumfanya kukosa maji ya matumizi pale nyumbani.

Maji ya matumizi kwa jirani

Hellen Cheptum akiwa na maafisa wa polisi nyumbani kwake Lityei kufuatia mkasa wa wanaume wawili kutumbukia kisimani. Picha|Oscar Kakai

Bi Cheptum alisema kuwa walienda kuomba maji ya matumizi kwa jirani.

“Niliomba maji kwa jirani na nikayatumia siku hiyo,” akasema Bi Cheptum.

Ilipofika Jumanne asubuhi, Bi Cheptum alikutana na Jonny akiwa na mwenzake mwingine kwenye barabara na mara moja akamwambia kuwa ndoo yake na kamba vilianguka kwenye kisima na hivyo hangeweza kuchota maji.

Alieleza kuwa wakati huo hakuwa na pesa za kuwalipa wale ambao wangeondoa vifaa hivyo.

Aliahidi kumuita Jonny baadaye afanye kazi hiyo pindi ambapo angepata pesa.

Lakini kulingana na mama huyo, Johny alisisitiza kwamba angefanya kazi hiyo wakati huo, kisha asubiri pesa baadaye.

Bi Cheptum alisema kuwa wawili hao walimfuata hadi kwenye boma lake.

Alithibitisha kuwa Jonny alitaka kulipwa Sh200 kwa kazi hiyo.

“Nilimwambia sina pesa lakini akasema nimpe Sh200 tu ama hata angefanya kazi hiyo bila malipo. Aliingia ndani ya shimo na kutoka.

Nilimwambia asiingie tena ikiwa aliona kuna hatari. Rafiki yake alimkataza lakini hakusikia na kuingia tena,” akaeleza Bi Cheptum.

Mwishowe, juhudi za mwanamume huyo raia wa Uganda ambaye amekuwa akiishi nchini kwa muda sasa, alishindwa kutoa vifaa hivyo.

Alianguka ghafla.

“Nilikuwa kwa mlango nikasikia kishindo cha akianguka. Nilikimbia kwa jirani na kumuita aokoe kisha tukapigia polisi simu. Kifo cha mtu wa pili pake kisimani kilitokea nikiwa nimejificha kwa uoga. Nilisikia watu wakipiga nduru,” alisema.

Mikasa hiyo miwili ilijiri huku serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi ikilaumiwa kwa kukosa kujiandaa vyema wakati wa majanga.

Ilielezwa kwamba waokoaji waliojitolea kuondoa miili hiyo walikuwa wakilemewa kutokana na kukosekana kwa oksijeni ndani ya kisima.

Wataalamu wa vifaa vya kusaka miili

Majirani wafurika katika makazi ya Hellen Cheptum kufuatia mkasa wa wanaume wawili kutumbukia kisimani na kufariki. Picha|Oscar Kakai

Kaunti ya Pokot Magharibi inakosa wataalamu na vifaa vya kusaka miili wakati wa majanga.

Ilishangaza kuwa kaunti za Pokot Magharibi na Trans-Nzoia huwa hazina mitungi ya oksijeni ya waokoaji na wataalamu hulazimika kuitoa katika kaunti ya Uasin Gishu.

Kulingana na wakazi, kumeripotiwa visa vingi vya watu kufa ndani ya visima, lakini maafisa wa kupambana na majanga huchelewa kufika katika eneo la mkasa.

Japo wakazi walidai kuwa wawili hao walikuwa walevi, walilaumu maafisa wa usalama, wakisema mwanamume wa pili hakufaa kuruhusiwa kuingia mle.

Bw Ibrahim Musa, mkazi, alisema lilikuwa ni kosa kumruhusu kuingia katika kisima cha mauti kwa kutaka fedha ilihali yeye sio mtaalamu.

“Maafisa ndio wa kulaumiwa… Walitukufukuza ilhali tulikuwa na maoni ambayo yangesaidia,” alisema Bw Musa.

Alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo haina vifaa na mashini za kutumika wakati wa majanga ya dharura kama kuondoa miili.

Mkazi mwingine, Bi Mercy Chepkiech, alisema alikuwa amekunywa pombe aina ya busaa na mtu wa kwanza kufariki ndani ya kisima hicho.

America Andiema, mkazi pia, alisema kuwa walikosa kufunga kamba kiunoni mwa mtu wa pili.

“Alitemremka kwenye kisima kutumia kamba ambayo mtu wa kwanza alitumia na kubaki mle ndani,” akasema Andiema.

Aliongeza kuwa matukio mengi sawa na mkasa huo, huripotiwa katika eneo hilo.

“Hatujui shetani gani ametufuata eneo hili. Mwaka 2023 watu wawili walifariki kwenye kisima katika mtaa huu,” akasema.

Naye Bw Isaiah Kisuri alitoa wito kwa serikali ya kaunti kununua vifaa vya kupambana na majanga.

“Hao watu wangeokolewa kama tungekuwa na vifaa maalumu. Tunataka maafisa wawe wakifika kwenye maeneo ya mikasa bila kupoteza muda,” alisema Bw Kisuri.

Naye Kirwa Chebos alisema ikiwa kweli walikuwa walevi, yalikuwa ni makosa kumtumia mlevi kuondoa mwili wa marehemu kisimani.
“Maafisa hawangeruhusu mtu mlevi kuingia kisimani,” akasema Bw Chebos.

Bi Fatuma Ramadhan Ndamwe alisema maafisa wanafaa kunyooshewa kidole cha lawama kufuatia vifo vya wanaume hao wawili.

Kikosi cha uokoaji kilikuwa kikiongozwa na Kamishna msadizi wa Mnagei (ACC) Bi Pamela Cheto Mwaka 2023, watu wawili walifariki ndani ya kisima kwenye kijiji hicho.

Miaka miwili iliyopita, wanafunzi watatu wa shule ya msingi ya Chewoyet walifariki ndani ya kisima.