Michezo

Wanavikapu wa Kenya kuvaana na Senegal Novemba 27

June 18th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANAVIKAPU wa Kenya Morans watafungua kampeni za Kundi B za kuwania taji la Afrika katika kipute cha FIBA AfroBasket mnamo Novemba 27 kwa kuvaana na Senegal.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Vikapu (FIBA), mahali pa kuandaliwa kwa kivumbi hicho cha vikosi vinne kitakachonogeshwa kwa mikondo miwili, patafichuliwa mwishoni mwa wiki hii baada ya wadau kuafikiana.

Pambano jingine la Kundi B litakaloandaliwa siku hiyo hiyo ambapo Morans watacheza ni lile litakalowakutanisha mabingwa mara 11 na watani wao wa tangu jadi katika mashindano ya Zone Six, Msumbiji.

Kenya wamepangiwa kupepetana na Angola mnamo Novemba 28 katika mchuano wao wa pili kabla ya kufunga mechi za makundi kwa kupimana ubabe na Msumbiji mnamo Novemba 29.

Mkondo wa pili ya kipute cha AfroBasket umeratibiwa kuanza Februari 19, 2021 kwa mechi itakayowakutanisha tena Kenya na Senegal. Baadaye, watashuka ugani kukabiliana na Angola mnamo Februari 20 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya Msumbiji mnamo Februari 22.

Kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya kimataifa, Morans ndio wanaokamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Wanashikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.

Jumla ya vikosi 20 vitapangwa katika makundi matano ya vikosi vinne kwa minajili ya mechi za raundi ya pili ya mchujo. Washindi watatu wa kwanza kutoka kila kundi watajikatia tiketi za kushiriki fainali za FIBA AfroBasket zitakazoandaliwa jijini Kigali, Rwanda.

Chini ya kocha Cliff Owuor, Kenya inalenga kunogesha fainali za kipute hicho cha haiba kubwa barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1993.

“Napania kuwaita kambini wanavikapu wangu wote pamoja na wale walioko ughaibuni kwa maandalizi ya mapema yatakayoweka hai matumaini yetu ya kujitwalia ubingwa wa AfroBasket. Ilivyo, sioni kizingiti kikubwa katika safari ya kufikia mafanikio hayo,” akasema Owuor.

Kati ya mikakati yake ya kujifua kwa kivumbi hicho, Owuor amefichua kwamba vijana wake wamepangiwa mechi za kirafiki dhidi ya Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Michuano hiyo itaanza pindi janga la corona litakapodhibitiwa vilivyo na mataifa hayo husika kulegeza kanuni za usafari.

Mnamo 1993, Morans waliambulia nafasi ya nne kwenye vikapu vya AfroBasket licha ya kuwa wenyeji wa kipute hicho jijini Nairobi.

Mnamo 2019, kikosi hicho kiliduwaza miamba wa bara la Afrika kwa kutinga fainali za kivumbi hicho nchini Mali japo ambapo walizidiwa maarifa na DR Congo.

Chini ya nahodha Griffin Ligare, Morans walifuzu kwa fainali baada ya kutawala kundi la washindani sita kwenye mchujo ulioandaliwa uwanjani Nyayo, Nairobi. Wakichuma nafuu kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani, Morans waliwabwaga Burundi, Eritrea, Sudan Kusini, Somalia na Tanzania.