Michezo

Wanavikapu wa 'majuu' wathibitisha kutambisha Morans kwenye fainali za FIBA Afro-Basket nchini Rwanda

October 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANAVIKAPU watatu wa kimataifa – Tyler Okari (Denmark), Joel Awich (Ufaransa) na Desmond Owili (Australia) watakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na timu ya taifa ya Kenya almaarufu Morans kwenye michuano ya Novemba 2020 ya kufuzu kwa fainali za FIBA Afro-Basket jijini Kigali, Rwanda.

Kocha Cliff Owuor wa Morans amethibitisha kwamba watatu hao watawasili humu nchini siku chache kabla ya kikosi kufunga safari ya kuelekea Rwanda mnamo Novemba 25.

Okari na Owili walikuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa Morans kwenye mechi za mchujo mnamo Januari mwaka huu. Kwa upande wake, itakuwa mara ya kwanza kwa Joel Awich ambaye ni mwanawe supastaa wa zamani wa humu nchini katika vikapu vya wanawake, Lynette Awich kuvalia jezi za timu ya taifa.

“Nimewasiliana nao na wamethibitisha kwamba watatua humu nchini siku chake kabla ya kikosi kuondoka,” akasema Owuor ambaye aliongoza Morans kuanza mazoezi kwa minajili ya kipute cha Afro-Basket mnamo Oktoba 13 uwanjani Nyayo.

Preston Bungei na Alonzo Ododa ambaye ni mwanawe mwanavikapu wa zamani wa kimataifa, Sebastien Ododa ni miongoni mwa wanavikapu tisa wanaochezea nje ambao Owuor amewaita kambini kukamilisha kikosi chake kinachojivunia wachezaji 10 wanaochezea klabu za humu nchini. Hao ni pamoja na nahodha Griffin Ligare, Joseph Khaemba, Faheem Juma, Victor Odendo, Eric Mutoro, Victor Ochieng na James Mwangi aliyekosa kivumbi cha Afro-Can nchini Mali mnamo Julai 2019 na michuano ya mchujo iliyoandaliwa jijini Nairobi mnamo Januari 2020.

Wakichuma nafuu kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani, Morans waliwabwaga Burundi, Eritrea, Sudan Kusini, Somalia na Tanzania kwenye mchujo huo ulioandaliwa uwanjani Nyayo.

Morans watafungua kampeni zao za Kundi B za kuwania taji la FIBA Afro-Basket dhidi ya Senegal mnamo Novemba 27. Kenya wamepangiwa kupepetana na Angola mnamo Novemba 28 katika mchuano wao wa pili kabla ya kufunga mechi za makundi kwa kupimana ubabe na Msumbiji mnamo Novemba 29.

Mkondo wa pili ya kipute cha Afro-Basket umeratibiwa kuanza Februari 19, 2021 kwa mechi itakayowakutanisha tena Kenya na Senegal. Baadaye, wanavikapu wa Owour watashuka ugani kukabiliana na Angola mnamo Februari 20 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya Msumbiji mnamo Februari 22.

Kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya kimataifa, Morans ndio wanaokamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Wanashikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.

Jumla ya vikosi 20 vitapangwa katika makundi matano ya vikosi vinne kwa minajili ya mechi za raundi ya pili ya mchujo. Washindi watatu wa kwanza kutoka kila kundi watajikatia tiketi za kushiriki fainali za FIBA Afro-Basket nchini Rwanda.

Chini ya Owuor, ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya APR nchini Rwanda, Morans wanalenga kunogesha fainali za FIBA Afro-Basket – kipute hicho cha haiba kubwa barani Afrika – kwa mara ya kwanza tangu 1993.

Mnamo 1993, Morans waliambulia nafasi ya nne kwenye vikapu vya Afro-Basket licha ya kuwa wenyeji wa kipute hicho jijini Nairobi. Mnamo 2019, kikosi hicho kiliduwaza miamba wa bara la Afrika kwa kutinga fainali za kivumbi hicho nchini Mali japo wakazidiwa maarifa na DR Congo.