Habari

Wanawake 2 wafariki kwa mkanyagano wa chakula cha msaada Kibra

April 11th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

WANAWAKE wawili walikufa usiku wa kuamkia Jumamosi kutokana na majeraha waliyopata kwenye mkanyagano uliotokea Ijumaa jioni wakati wakazi wa mtaa Kibra, Nairobi walipokuwa wakigawiwa chakula cha msaada.

Mkanyagano huo ulidhihirisha wazi mahangaiko ambayo maskini wanapitia wakati huu ambapo shughuli nyingi za kazi zimekwama kwa sababu ya janga la corona.

Kufuatia kisa hicho, serikali jana ilipiga marufuku watu na mashirika ya kibinafsi kusambaza vyakula na bidhaa za msaada kwa wenye mahitaji.

Badala yake iliagiza misaada yote itolewe kupitia kwa Hazina ya Dharura ya Covid-19, magavana na makamishna wa kaunti pekee.

Inaaminika sehemu ya misaada iliyokuwa ikitolewa katika ofisi za Naibu Kamishna wa Kibra ni ile iliyopelekwa Alhamisi na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga.

“Kuna wanawake watatu waliojeruhiwa watu waliposukumana na kukanyagana wakati wa kugawiwa chakula cha msaada katika ofisi za Naibu Kamishna. Baadaye wawili wao walikufa wakipelekwa hospitalini,” alisema mkazi Esther Auma aliyeshuhudia kisa hicho.

Mkuu wa polisi eneo la Kibra Andrew Musaisi alithibitisha wanawake hao walikufa saa chache baada ya mkanyagano.

Watu wengine kadhaa walijeruhiwa kwenye kizaazaa hicho, ambacho wanaharakati walisema kilisababishwa na ukosefu wa utaratibu mwema wa kugawa chakula cha misaada.

“Watu walikusanyika eneo moja kinyume na maagizo ya serikali. Inashangaza kisa hiki kilitokea katika ofisi ya Naibu Kamishna ambaye anafaa kutekeleza masharti ya serikali,” alisema mwanaharakati wa Kibra Isa Salim.

Chama cha ODM kilimwondolea lawama Bw Odinga kikisema hakuwa na jukumu la kusambaza misaada aliyotoa.

“Chakula cha msaada kilipelekwa katika afisi ya serikali Kibra na kikapokewa na Kamishna wa Kaunti Ndogo. Lilikuwa jukumu lake kutafuta njia ya kusambazia wananchi chakula hicho. Kwa hivyo ni yeye anayefaa kulaumiwa kwa vurugu zozote zilizotokea, wala si Bw Odinga,” akasema mkurugenzi wa mawasiliano wa chama hicho Philip Etale.