Habari Mseto

Wanawake Kiambu wahimizwa kuzingatia teknolojia mpya

October 25th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KIKUNDI kimoja cha wanawake Kaunti ya Kiambu kimejitolea kubuni njia rahisi ya kupata umeme kwa kutumia teknolojia rahisi.

Wakiwa katika kikundi kinachojulikana kama Rural Women in Energy Umbrela, wamebuni njia rahisi ya kupikia kutumia biogesi na teknolojia ya bricades ili kujiepusha na utumizi wa kuni vijijini na ambazo zinachangia katika ukataji holela wa miti.

Wanawake hao walisema iwapo watapewa ufadhili wa kifedha na kuhamasishwa vyema kuhusu teknolojia hiyo, bila shaka watapiga hatua kubwa ambapo wataweza pia kuchangia kikamilifu katika kuendana na ajenda nne muhimu za serikali.

Bi Mary Rigathi wa kikundi hicho alisema cha muhimu kwao ni kupewa mwongozo na ufadhili ili waweze kujikwamua kutoka kwa umaskini.

“Sisi wanawake tunatamani sana kuungana pamoja na kufanya kilimo na ufugaji kwa njia kubwa, lakini jambo linaloponza juhudi zetu ni mtu wa kutupatia mwongozo na hamasisho,” alisema Bi Rigathi.

Kikundi hicho cha wanawake hao kutoka mashinani walitunukiwa tuzo mwaka 2018 kwa juhudi zao za kubuni njia rahisi ya kupika kutumia teknolojia rahisi ya biogesi.

Mtaalamu wa teknolojia ya vyombo tofauti Bw James Ngomeli alisema wanawake wana umuhimu mkubwa katika jamii na ni lazima wahusishwe katika maamuzi muhimu kuhusu teknolojia mpya ya kisasa.

Alisema mabomba ya maji na sola za kutumia miale ya jua zinastahili kusambazwa mashinani ili waweze kuhamasishwa jinsi ya kutumia wakiwa vijijini kwa sababu ni teknolojia rahisi.

“Tukiwaweka mbele wanawake katika maswala ya kiteknolojia, bila shaka mafanikio ya ajenda nne muhimu za serikali yatakuwa ya kufana,” akasema.

Alisema umefika wakati mambo yaliyoendeshwa kwa mikono tu yachukue mkondo wa kukumbatia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha mambo.

Bi Mary Wairimu ambaye ndiye mwenyekiti wa kikundi hicho alisema ni vyema wanawake wa mashinani kukumbatia mafunzo hayo ya kiteknolojia kwa sababu asilimia kubwa ya vyombo vinavyotumika kiteknolojia vinaendehswa na wanawake hao kutoka vijijini.

“Mimi kama mwenyekiti nitakuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba asilimia kubwa ya wanawake wanapewa nafasi ya kuelewa mambo yanayoambatana na teknolojia ya kisasa. Sisi wanawake tunastahili kuwa mstari wa mbele ili tujiendeleze na hali ya mabadiliko yanayoshuhudiwa kila mahali,” alisema Bi Wairimu.

Alisema watazidi kushirikiana pamoja ili kufanikisha malengo yao na kuona ya kwamba kila mwanamke anajisimamie katika maisha yake kwa njia inayostahili.